Dakta Ali Larijani: Iran ina uwezo wa kukabiliana na vikwazo
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria vikwazo vya kidhulma vya Marekani dhidi ya Iran ambavyo vinakinzana pia na sheria na kanuni za kimataifa na kusisitiza kuwa, taifa hili lina uwezo wa kukabiliana na vikwazo hivyo.
Dakta Ali Larijani amebainisha kwamba, licha ya makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) kuungwa mkono na madola makubwa duniani na kadhalika Umoja wa Mataifa, lakini Rais Donald Trump wa Marekani amechukua hatua ya upande mmoja ya kuiondoa nchi yake katika makubaliano hayo.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema bayana kwamba, hatua yya Marekani ya kujiondoa katika makubaliano hayo ya kimataifa ambayo yaliidhinishwa pia na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imethibitisha kwamba, Washington katu haiheshimu makubaliano yoyote yale.
Aidha Larijani amesisitiza kuwa, Rais Donald Trump amekuwa akizungumza kwa lugha mbaya na isiyo na adabu hata na mataifa ambayo yametoa msaada mkubwa kwa Marekani, ambayo yamenunua silaha za Washington zenye thamani ya dola bilioni 110 na ambayo yamesaidia kiasi cha dola bilioni 50 kwa ajili ya miundo mbinu ya Marekani.
Spika wa Bunge la Iran ameashiria pia kuundwa baadhi ya miungano midogo katika eneo la Mashariki ya Kati eti kwa ajili ya kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamuu ya Iran na kusema bayana kwamba, nchi hizo hazina ujasiri na ubavu wa kuchukua hatua yoyote ile dhidi ya taifa hili lililopiga hatua katika nyanja mbalimbali.