Zarif: Iran itanawiri na haitatoa muhanga mamlaka yake ya kujitawala
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif ametupilia mbali vitisho vya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kuwa taifa la Iran litakumbwa na njaa.
Zarif amesisitiza kuwa si tu kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitakumbwa na masaibu bali hata itaweza kunawiri pamoja na kuwepo vikwazo vya Marekani.
Katika ujumbe kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter Jumamosi, Zarif amesema tishio la wazi la Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo kuwa Washington itahakikisha kuwa Wairani wanakumbwa na njaa ni 'jinai dhidi ya binadamu' na jaribio la kulazimisha matakwa ya Marekani kwa Iran. Zarif amesema, Pompeo, kama wenzake waliomtangulia, hatimaye atafahamu kuwa, licha ya njama za Marekani, si tu kuwa taifa la Iran halitakumbwa na masaibu bali pia litaweza kustawi pasina kutoa muhanga mamlaka yake ya kujitawala.
Jana Jumamosi pia Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kuwa, wananchi wa Iran wameishinda mipango na njama za Marekani kwa kusimama kwao kidete. Rais Rouhani alisema kuwa, shabaha kuu ya Marekani ya kuiwekea Iran vikwazo visivyo halali na kuulenga mfumo wa benki, usafirishaji mafuta na baadhi ya bidhaa za taifa hili zinazosafirishwa nje ya nchi, ni kutaka kuweka athari mbaya na hasi katika maisha ya wananchi wa Iran.

Katika mahojiano na BBC, Pompeo alisema wakuu wa Iran wanapaswa kutii matakwa ya Marekani iwapo wanataka Wairani wapate chakula. Tarehe 8 Mei mwaka huu, rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kujitoa nchi yake kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kurejesha tena vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran. Awamu ya kwanza ya vikwazo hivyo ilianza kutekelezwa tarehe 7 Agosti, na awamu ya pili ilianza kutekelezwa rasmi Jumatatu ya tarehe 5 Novemba.