Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Uingereza wakutana mjini Tehran
Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uingereza leo wamekutana na kufanya mazungumzo hapa mjini Tehran kuhusiana na masuala muhimu ya kieneo ukiwemo ulazima wa kuharakishwa kuhitimishwa vita nchini Yemen pamoja na matukio yanayojiri sasa katika Mashariki ya Kati.
Dakta Muhammad Javad Zarif na mgeni wake Jeremy Hunt vilevile wamezungumza na kubadilishana mawazo kuhusiana na njama zilizo dhidi ya ushirikiano wa Tehran na London likiwemo suala la kuanzishwa mfumo mpya wa mabadilishano ya kifedha na Ulaya unaojulikana kama SPV kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la ushirikiano wa kibiashara katika fremu ya makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Baada ya kumaliza kufanya mazungumzo na Dakta Zarif, Jeremy Hunt, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza amekutana pia na kufanya mazungumzo na Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran.
Hii ni safari ya kwanza kufanywa na Jeremy Hunt hapa Tehran baada ya kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza. Safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza hapa Tehran inafanyika baada ya kutekelezwa duru ya pili ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na inaonekana kuwa suala la mfumo maalumu wa miamala ya kifedha (SPV) uliopendekezwa na Ulaya kwa ajili ya kudhamini maslahi ya Iran katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na hatua nyingine za Ulaya katika uwanja huo ni kati ya mambo ambayo huenda yakajadiliwa na kuchunguzwa katika ziara hii ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza mjini Tehran.