Salehi: Msimamo wa Marekani wa kujitoa katika JCPOA si wa maana
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49785-salehi_msimamo_wa_marekani_wa_kujitoa_katika_jcpoa_si_wa_maana
Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Iran amesema kuwa msimamo wa Mrekani wa kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA si wa maana na ni kwamba, msimamo huo unaonesha jinsi Marekani isivyo na mwamana katika ahadi zake za kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 26, 2018 23:11 UTC
  • Salehi: Msimamo wa Marekani wa kujitoa katika JCPOA si wa maana

Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Iran amesema kuwa msimamo wa Mrekani wa kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA si wa maana na ni kwamba, msimamo huo unaonesha jinsi Marekani isivyo na mwamana katika ahadi zake za kimataifa.

Dk Ali Akbari Salehi alisema hayo jana (Jumatatu) katika semina ya tatu ya ushirikiano wa kimataifa wa nyuklia baina ya Iran na Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji.

Amesema, ni jambo la kustaajabisha sana kuona mantiki iliyotumiwa na Marekani katika kujitoa kwenye mapatano hayo ya nyuklia wakati Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) umeshatoa ripoti 13 za kuthibitisha kuwa Iran imeheshimu kikamilifu makubaliano hayo.

Semina ya ngazi za juu ya ushirikiano wa kimataifa wa nyuklia baina ya Iran na Umoja wa Ulaya mjini Brussels Ubelgiji, Jumatatu, Novemba 26, 2018

 

Amesema, Tehran ina nia ya kweli ya kuendelea kuimarisha na kupanua ushirikiano wake na Umoja wa Ulaya katika masuala ya nyuklia kwani maendeleo yoyote yatakayopatikana kwenye jambo hilo ni kwa manufaa ya pande mbili na jamii nzima ya kimataifa.

Vile vile ameelezea matumaini yake kuhusu kustawi zaidi ushirikiano baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya katika masuala ya nyuklia na kuongeza kuwa, usalama wa nishati ya nyuklia ni katika mambo yanayopewa kipaumbele kikubwa na Iran kwani jambo hilo linasaidia sana katika uimara wa usalama kwenye mfumo wa fueli nyuklia.

Semina ya Tatu ya Kimataifa ya Ushirikiano wa Nyuklia baina ya Iran na Umoja wa Ulaya ilianza jana Jumatatu huko Brussels Ubelgiji na inamalizika leo Jumanne.