Iran na Uturuki zahimiza kufanikishwa biashara ya dola bilioni 30 baina yao
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49858-iran_na_uturuki_zahimiza_kufanikishwa_biashara_ya_dola_bilioni_30_baina_yao
Maspika wa mabunge ya Iran na Uturuki wamesisitizia haja ya kufanikishwa biashara ya dola bilioni 30 baina ya nchi zao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 30, 2018 01:03 UTC
  • Iran na Uturuki zahimiza kufanikishwa biashara ya dola bilioni 30 baina yao

Maspika wa mabunge ya Iran na Uturuki wamesisitizia haja ya kufanikishwa biashara ya dola bilioni 30 baina ya nchi zao.

Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) jana jioni alionana na Spika wa Bunge la Uturuki, Binali Yıldırım, pambizoni mwa kikao cha 11 cha Baraza Kuu la Mabunge ya Asia mjini Istanbul na kusisitiza kuwa, Iran na Uturuki ni washirika wawili muhimu wa kiuchumi katika eneo hili. Amesema, nchi zote hizi mbili zinahitajia sana kuimarisha ushirikiano baina yao hasa katika kipindi hiki cha vikwazo.

Larijani ameongeza kuwa, kitendo cha Marekani cha kutumia sarafu ya dola kama silaha baridi hakikubaliki kabisa na kwamba hatua hiyo ya Marekani imezifanya nchi zote zifikirie kutumia fedha zao wenyewe kufanyia mabadilishano ya kifedha na kiuchumi.

Kikao cha 11 cha Baraza Kuu la Mabunge ya Asia

 

Vile vile amesema, sababu kuu ya kuendelea machafuko na ukosefu wa amani katika nchi za Afghanistan, Iraq, Syria, Yemen na Libya ni Marekani na kusisitiza kuwa, shabaha kuu ya Washington ni kuulinda utawala wa Kizayuni wa Israel na kulisahaulisha suala la Palestina lakini kamwe haitofanikiwa kwenye njama yake hiyo.

Kwa upande wake, spika wa bunge la Uturuki amelaani hatua ya Marekani ya kutumia sarafu ya dola kama silaha na kuongeza kuwa, kitendo hicho cha Marekani ni kinyume cha taratibu za kimataifa.

Kikao cha 11 cha siku tatu cha Baraza Kuu la Mabunge ya Asia (APA) kilianza jana jioni mjini Istanbul Uturuki chini ya kaulimbiu ya kuimarisha ustawi wa kiuchumi wa Asia kikishirikisha wajumbe kutoka nchi 23 ikiwemo Iran.