Safari ya Uturuki ya Rais Rouhani; Mwanzo Mpya wa Ushirikiano wa Kistratijia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i50294-safari_ya_uturuki_ya_rais_rouhani_mwanzo_mpya_wa_ushirikiano_wa_kistratijia
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana Jumatano aliwasili mjini Ankara nchini Uturuki akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa akiitikia mwaliko wa Rais Recep Tayyip Erdoğan wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 20, 2018 03:49 UTC
  • Safari ya Uturuki ya Rais Rouhani; Mwanzo Mpya wa Ushirikiano wa Kistratijia

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana Jumatano aliwasili mjini Ankara nchini Uturuki akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa akiitikia mwaliko wa Rais Recep Tayyip Erdoğan wa nchi hiyo.

Ajenda muhimu zaidi ya safari hiyo ni kufanyika Kikao cha Tano cha Baraza Kuu la Kistratijia la Ushirikiano wa Iran na Uturuki chini ya uwenyekiti wa marais wa nchi mbili.

Uhusiano wa Iran na Uturuki umekuwa ukiimarika katika miaka ya hivi karibuni. Pendekezo la kuunda Baraza Kuu la Kistratijia la Ushirikiano wa Iran na Uturuki lilitolewa katika safari ya kwanza ya Rais Rouhani nchini Uturuki na kwa msingi huo marais wa nchi mbili wameweka lengo la biashara yenye thamani ya dola bilioni 30 kwa mwaka baina ya nchi mbili.

Hadi sasa kumefanyika vikao vinne vya Baraza Kuu la Kistratijia la Ushirikiano wa Iran na Uturuki na vikao hivyo vimefanyika katika mikutano ya marais wa nchi mbili na kufikia mapatano muhimu.

Kikao cha Tano cha Baraza Kuu la Kistratijia la Ushirikiano wa Iran na Uturuki kinafanyika leo Alhamisi katika mazingira mazuri ya uhusiano wa nchi mbili. Kutumia ipasavyo uwezo uliopo katika uhusiano wa kisiasa na kiuchumi wa Iran na Uturuki katika kustawisha ushirikiano ni nukta yenye umuhimu mkubwa.

Iran iko tayari kuandaa mazingira yanayohitajika ili kuimarisha ushirikiano wa nchi mbili kwa kuwakutanisha pamoja wadau wa masuala ya uchumi wa Iran na Uturuki. Ni wazi kuwa kuna vizingti katika mchakato wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili, hasa uhusiano wa kiuchumi baina ya Iran na Uturuki na hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa kuondoa vizingiti hivyo.

Rais Hassan Rouhani (kushoto) na Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amenukuliwa akisema kufanyika Kikao cha Tano cha Baraza Kuu la Kistratijia la Ushirikiano wa Iran na Uturuki ni fursa nzuri ya kuimarisha uhusiano wa Tehran na Ankara. Vilevile ameashiria udharura wa kuwepo jitihada za kuimarisha ushirikiano na kuwaunga mkono wadau wa kiuchumi wa nchi mbili na kusema: "Kustawisha uhusiano na Iran ni jambo lenye umuhimu wa kistratijia kwa Uturuki.

Duru za habari nchini Uturuki zinadokeza kuwa, ni nukta chanya na muhimu kuwa safari ya Rais Rouhani nchini humo inafanyika baada ya mapatano ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran, Uturuki na Russia mjini Geneva kuhusu suala la kuandikwa katiba mpya ya Syria.

Ali Najafi Khoshroverdi, Msemaji wa Tume ya Usalama wa Taifa katika Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, amesema kuwa safari ya Rais Rouhani nchini Uturuki ni fursa nzuri ya kufanya mazungumzo ya kistratijia katika kiwango cha juu hasa kwa kuzingatia migogoro na matatizo yaliyopo katika kanda hii. Ameongeza kuwa: "Mazungumzo hayo yanaweza kuondoa kisingizio kinachotumiwa na madola ajinabi kuingilia mambo ya eneo hili mbali na kuwa hali mpya iliyopo Iran inazidisha umuhimu wa kufanyika mazungumzo ya kistratijia kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi."

Sarafu ya Lira ya Uturuki. Iran na Uturuki zinapanga kutumia sarafu zao katika biashara

Hakuna shaka kuwa kuna umuhimu wa kuimarishwa ushirikiano wa kistratijia na mshikamano wa kisiasa baina ya Iran na Uturuki. Aidha kutiwa saini mapatano ya mabadilishano ya kifedha na kibenki ni kati ya nukta muhimu ambazo zinasisitizwa na wakuu wa nchi mbili. Kuhusiana na suala hilo Erdogan amesisitiza kuwa, sarafu za kitaifa za nchi mbili zitumike katika mabadilishano ya kiuchumi na ni wazi kuwa, nukta hii inaweza kuwa sababu ya kuimarishwa uhusiano wa kiuchumi baina ya Tehran na Ankara.

Kwa muda mrefu Iran imekuwa ikikabiliana na uhasama pamoja na vikwazo vya Marekani lakini sasa pia nchi kama vile Uturuki na Russia nazo zinakabiliwa na mashinikizo na vikwazo vya Marekani.

Kwa msingi huo mapatano na maelewano ya Iran na Uturuki katika masuala mbalimbali ni muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kieneo. Safari ya Rais Rouhani nchini Uturuki kushiriki katika Kikao cha Tano Baraza Kuu la Kistratijia la Ushirikiano wa Iran na Uturuki ni fursa muhimu kwa ajili ya kufikia malengo yanayokusudiwa na pande mbili katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano.