Dec 30, 2018 14:37 UTC
  • Iran yalaani shambulizi la kigaidi dhidi ya watalii nchini Misri

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani shambulizi la kigaidi la hivi karibuni lililopelekea kuuawa watalii kadhaa huko nchini Misri.

Bahram Qassemi ameitaja jinai hiyo kama ugaidi pofu na kusema kuwa shambulizi hilo linapasa kulaaniwa vikali. Amesema hujuma hiyo dhidi ya watalii waliokuwa wakienda kutembelea eneo la kihistoria ni uhaini na kitendo kisichokubalika hata chembe.

Hapo juzi, watalii watatu wa Vietnam na raia mmoja wa Misri waliuawa baada ya bomu lililotegwa kando ya barabara kuripukia basi lililokuwa likifanya safari ya kitalii karibu na Mapiramidi ya Giza nje kidogo ya mji mkuu wa Misri, Cairo. Basi hilo lilikuwa limebeba watu 16 wakiwemo watalii 14.

Katika kulipiza kisasi, maafisa usalama wa Misri wameripotiwa kuwaua watu 40 wanaotuhumiwa kuhusika na shambulizi hilo la juzi jioni.

Basi la watalii lililoshambuliwa

Misri kwa muda mrefu sasa imekuwa ikishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi yenye silaha dhidi ya raia na pia wanajeshi na maafisa usalama wa serikali.

Mashambulio hayo yameongezeka baada ya rais wa sasa Abdel Fattah el Sisi kushika hatamu za uongozi mwaka 2014 baada ya kuongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyompindua Mohammad Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri.

 

Tags