Zarif: Hakuna dola linaloweza kudai kuwa limehodhi nguvu zote za dunia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hakuna taifa lolote linaloweza kudai kuwa limehodhi nguvu zote za dunia katika enzi hizi, na kusisitiza kwamba zama za dola moja kufanya maamuzi kwa niaba ya mataifa kadhaa zimepitwa na wakati.
Mohammad Javad Zarif amesema hayo leo mjini Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran na kubainisha kuwa, "Hii leo, taifa moja haliwezi kuchukua maamuzi kwa niaba ya nchi nyingine dunia. Nguvu na uwezo umesambaa na kuenea katika nchi tofauti duniani."
Dakta Zarif amesema ni makosa makubwa kudhani kuwa katika dunia ya leo, madola eti yenye nguvu na uwezo kupindukia (Superpowers) yangalipo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria matamshi ya kejeli na ya kudhalilisha ya Rais Donald Trump, aliyesema kuwa iwapo Marekani itaacha kuipa himaya Saudi Arabia, basi taifa hilo la Kiarabu halitabaki hai kwa zaidi ya wiki moja; na kubainisha kuwa, "Fahari yetu kubwa hii leo ni kwamba, hakuna mtu yeyote anaweza kuthubutu kudai kuwa iwapo hatatuunga mkono kwa wiki moja, basi tutaanza kuzungumza Kiingereza, Kiarabu na Kirusi."
Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inategemea uwezo wake wa ndani katika kujidhaminia usalama na pia ustawi wa kiviwanda.
Dakta Zarif amekumbusha kuwa, "Makubaliano ya Iran na Uturuki katika mazungumzo ya Astana yalipunguza taharuki nchini Syria, jambo ambalo Marekani na Russia zilishindwa kufikia kwa zaidi ya miaka miwili. Kupungua taharuki na mapigano nchini Syria kumeielekeza nchi hiyo ya Kiarabu katika njia ya amani, na jambo hilo linaashiria nafasi athirifu ya Iran katika eneo."