CNN: Iran haioneshi kuwa na muelekeo wa kusalimu amri mbele ya Marekani
Kanali ya televisheni ya CNN ya Marekani ambayo imeyaakisi maandamano ya leo ya Bahman 22 (Februari 11) ya mjini Tehran ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, imeeleza katika ripoti yake kuwa, Iran haioneshi kuwa na muelekeo wa kusalimu amri mbele ya Marekani.
Huku ikiakisi maandamano ya leo kwa anuani ya "Maadhimisho ya mwaka wa 40 wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran", CNN imetangaza kuwa: Iran ingali inaonesha kuwa haina nia ya kusalimu amri mbele ya Marekani na mashinikizo ya kimataifa.
Maandamano ya kuadhimisha mwaka wa 40 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalianza leo asubuhi kwa wakati mmoja nchini kote katika miji zaidi ya elfu moja na vijiji elfu kumi.
Wananchi wa Iran waliokuwa wamebeba bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walisikika wakipaza sauti na kutoa nara za "Mauti kwa Marekani" na "Mauti kwa Israel".
Mnamo siku ya Ijumaa, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyed Ali Khamenei aliuelezea utawala wa Marekani kuwa ni dhihirisho la shari, ukatili, utumiaji mabavu, uzushaji migogoro na uwashaji moto wa vita na akabainisha kwa kusema: "Ili viongozi wa Marekani wabainikiwe vizuri akilini mwao, tunasisitiza kwamba, sisi hatuna tatizo lolote na wananchi wa Marekani; na maana ya mauti kwa Marekani, ni mauti kwa watawala wa Marekani, ambapo katika kipindi hiki ni mauti kwa Trump, Pompeo na Bolton."
Jumla ya waandishi wa habari, wapiga picha na wachukuaji filamu 6,500 wa ndani na nje ya Iran, ambapo zaidi ya 300 kati yao ni wa kigeni wamefanya kazi ya kuakisi matukio ya maadhimisho ya mwaka wa 40 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Mbali na mamilioni ya wananchi, maadhimisho yaliyofanyika katika mji mkuu Tehran yamehudhuriwa pia na wageni kutoka nje ya nchi wakiwemo shakhsia mbali mbali wa kisiasa, kidini, wanamichezo na wanataaluma kutoka Marekani, Ufaransa, Uingereza, Ireland na Venezuela.../