Rouhani: Iran itasaidia kuijenga upya Syria na kuirejeshea utulivu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51806-rouhani_iran_itasaidia_kuijenga_upya_syria_na_kuirejeshea_utulivu
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kushiriki katika utekelezaji wa mipango itakayoainishwa na serikali ya Syria katika kuijenga upya nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 26, 2019 04:19 UTC
  • Rouhani: Iran itasaidia kuijenga upya Syria na kuirejeshea utulivu

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kushiriki katika utekelezaji wa mipango itakayoainishwa na serikali ya Syria katika kuijenga upya nchi hiyo ya Kiarabu.

Rais Rouhani aliyasema hayo katika mazungumzo yake na na Rais Bashar al Assad wa Syria hapa mjini Tehran jana Jumatatu na kuongeza kuwa, serikali ya Iran kama ilivyokuwa huko nyuma, itaendelea kuisaidia na kushirikiana na Syria katika juhudi zake za kurejesha amani na utulivu katika nchi hiyo iliyoshuhudia vita na uharibifu mkubwa kwa miaka kadhaa sasa.

Rais wa Iran amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu iko tayari wakati wote kuimarisha ushirikiano wake wa kiuchumi na Syria katika kiwango cha kiistratijia na kuongeza kuwa, Tehran iko tayari kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Damascus katika nyuga mbalimbali.

Amesema ushirikiano wa pande kadhaa wa nchi za Mashariki ya Kati umechangia pakubwa katika kurejesha usalama na uthabiti katika eneo hili.

Rais wa Syria alipokutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei

Dakta Hassan Rouhani ameongeza kuwa, Tehran itashirikiana na Damascus katika mchakato wa kurejesha wakimbizi wa Syria katika nchi yao.

Kwa upande wake, Rais Bashar al Assad amesema kuwa, serikali na taifa la Syria kwa ujumla linaishukuru Iran kwa kuwaunga mkono Wasyria hususan katika vita dhidi ya ugaidi. Hali kadhalika ameipongeza serikali ya Tehran kwa jitihada zake za kurejesha amani na utulivu sio tu nchini Syria bali katika eneo la Mashariki ya Kati kwa ujumla.

Rais wa Syria hapo jana alikutana na kufanya mazungumzo pia na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ambaye alisisitiza kuwa, Iran inalihesabu suala la kuiunga mkono Syria kuwa ni sawa na kuunga mkono muqawama na inaona fakhari kwa jambo hilo.