Iran yapiga marufuku ndege za Boeing 737 Max kuruka katika anga yake
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepiga marufuku ndege ya Marekani aina ya Boeing 737 Max kutumia anga yake kufuatia kuanguka ndege mpya ya aina hiyo ya Shirika la Ndege la Ethiopia hivi karibuni.
Shirika la Safari za Anga la Iran limetoa taarifa leo Ijumaa ya kupiga marufuku ndege hizo za Marekani kutumia anga ya nchi hii na kujiunga na orodha ya nchi kadhaa duniani ambazo zimeshatangaza kupiga marukufu ndege hizo.
Mkuu wa Ofisi ya Uhusiano Mwema wa shirika hilo la Iran, Reza Jafarzadeh amesema: "Tumepiga marufuku ndege ya Boeing Max kuruka katika anga yetu kama ambavyo nchi nyingine kadhaa zimefanya."
Nchi za Umoja wa Ulaya tayari zimepiga marufuku ndege za aina hiyo zinazotengenezwa Marekani kupita katika anga zao.
Nchi ambazo zimesitisha kwa muda operesheni za ndege ya Boeing 737 Max ni pamoja na Ethiopia, China, Singapore, Indonesia , Brazil na Argentina.
Ndege ya Boeing 737 Max ya Ethiopia nambari ET302 ilianguka Jumapili iliyopita dakika chache tu baada ya kuondoka kwenye uwanja wa ndege wa Addis Ababa ambapo watu wote 157 waliokuwamo walipoteza maisha, ikiwa ni chini ya miezi mitano baada ya Lion Air Boeing 737 Max kunguka muda mfupi baada ya kuondoka Jakarta, Indonesia, na kuwauwa watu wote 189 waliokuwa ndani yake.