Dakta Zarif: Saudi Arabia bado hamjachelewa, sitisheni vita dhidi ya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i52425-dakta_zarif_saudi_arabia_bado_hamjachelewa_sitisheni_vita_dhidi_ya_yemen
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameihutubu Saudi Arabi na washirika wake akiwanasihi kwamba, bado hawajachelewa kusimamisha jinamizi lililotokana na vita dhidi ya nchi masikini ya Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 26, 2019 22:11 UTC
  • Dakta Zarif: Saudi Arabia bado hamjachelewa, sitisheni vita  dhidi ya Yemen

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameihutubu Saudi Arabi na washirika wake akiwanasihi kwamba, bado hawajachelewa kusimamisha jinamizi lililotokana na vita dhidi ya nchi masikini ya Yemen.

Dakta Muhammad Javad Zarif amesema hayo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kusema kuwa: Saudi Arabi na washirika wake walikataa pendekezo la mpango wa amani wa Iran kwa ajili ya Yemen wa Aprili 2015 na wakadai kwamba, watapata ushindi katika kipindi cha wiki tatu tu.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  ameongeza kuwa, wakati huu wa kuanza mwaka wa tano wa vita hivi vya fedheha, inapasa kukumbusha kwamba, waliaonzisha vita hivyo bado hawajachelewa sana kuchukua hatua ya kusitisha hujuma hiyo ya kijeshi.

Saudi Arabia na washirikan wake wameendelea kuishambulia Yemen licha ya miito ya walimwengu ya kusimamishwa vita hivyo

Itakumbukwa kuwa Saudia kwa kushirikiana na Marekani, Israel, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi na Kiarabu ilianzisha mashambulizi makali ya kila upande dhidi ya Yemen hapo mwezi Machi 2015 sambamba na kuizingira nchi hiyo masikini ya Kiarabu kwa pande za nchi kavu, baharini na angani.

Vita vya Saudia na washirika wake nchini Yemen hadi sasa vimepelekea mauaji ya zaidi ya watu elfu 16, makumi ya maelfu kujeruhiwa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Hata hivyo Saudia na washirika wake wameshindwa kabisa kufikia malengo yao haramu ndani ya nchi hiyo kutokana na mapambano ya Wayemen.