Qassemi: Marekani ifahamu haiwezi kupora utajiri wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i52456-qassemi_marekani_ifahamu_haiwezi_kupora_utajiri_wa_iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria hukumu ya Mahakama ya Luxembourg ambayo imekataa ombi la Marekani la kuchukua udhibiti wa mali za Benki Kuu ya Iran na kusema: "Marekani inapaswa kufahamu kuwa, kwa kutumia hadaa haiwezi kupora utajiri na milki za Wairani.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Mar 28, 2019 03:31 UTC
  • Qassemi: Marekani ifahamu haiwezi kupora utajiri wa Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria hukumu ya Mahakama ya Luxembourg ambayo imekataa ombi la Marekani la kuchukua udhibiti wa mali za Benki Kuu ya Iran na kusema: "Marekani inapaswa kufahamu kuwa, kwa kutumia hadaa haiwezi kupora utajiri na milki za Wairani.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameendelea kusema kuwa zile zama za Marekani kuzidhulumu na kuzikandamiza nchi zingine kwa kutumia tuhuma zisizo na msingi sasa zimefika ukingoni. Ameongeza kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani anapaswa kufahamu kuwa Iran na watu wake adhimu na werevu ni tafauti na wengine ambao huikabidhi Marekani utajiri wao ili kukodisha usalama na uungaji mkono.

Qassemi amebaini kuwa, Marekani imeshindwa mara kadhaa na taifa la Iran katika mapambano ya kisheria na kisiasa na hivyo inapaswa kufahamu kuwa, itaendelea kushindwa na kusambaratishwa na serikali ya Iran pamoja na taifa la Iran. 

Ikumbukwe kuwa siku ya Jumatano, Mahakama ya  Luxembourg  imetupilia mbali ombi la Marekani la kutaka kuchukua udhibiti wa dola bilioni 1.6 za Iran na kuzitumia kuwapa waathirika wa hujuma za kigaidi za Septemba 11 mwaka 2001.

Mahakama hiyo imetangaza kuwa, nyaraka zilizowasilishwa na Marekani katika kesi hiyo dhidi ya Benki Kuu ya Iran zinakiuka sheria za kimataifa.

Mahakama moja ya Marekani ilikuwa imewasilisha kesi ya kutaka fedha za Iran zilizoko nchini Luxembourg  zichukuliwe na Marekani kwa ajili ya kuwalipa fidia waathirika wa hujuma za Septemba 11.

Benki ambayo Iran imeweka fedha zake nchini Luxembourg 

Marekani ilikuwa imetoa madai ya kichekesho kuwa eti Iran ilihusika na hujuma za Septemba 11, madai ambayo ni kinyume kabisa cha taarifa za kijasusi zilizopo na hata ni kinyume cha ripoti ya uchunguzi wa Bunge la Marekani, Kongresi.

Nyaraka za ripoti ya  Kamati ya Uchunguzi ya Kongres iliyochapishwa mwaka 2017 inaonyesha kuwa, watu 15 kati ya 19 walioteka nyara ndege na kuzitumia katika hujuma za Septemba 11 walikuwa ni raia wa Saudi Arabia na wawili wengine walikuwa raia wa Imarati ambao walipata msaada wa kifedha na kilojistikia kutoka kwa maafisa wa ngazi za juu wa Saudia na Imarati. Tawala hizo mbili ni waitifaki wakuu wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi.