IAEA yasisitiza tena kuwa Iran imefungamana na JCPOA
Kwa mara nyingine tena Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amethibitisha kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefungamana na kutekeleza majukumu yake kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Yukia Amano aliyasema hayo jana Jumanne na kusisitiza kuwa, Iran inaendelea kutekeleza ahadi na majukumu yake kuhusiana na miradi yake ya nyuklia. Amano ameongeza kuwa IAEA imeweza kutekeleza ukaguzi katika vituo vya nyuklia vya Iran bila vizingiti vyovyote.
Hii ni mara ya 16 kwa IAEA kuthibitisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza ahadi zake kuhusiana na makubaliano ya JCPOA.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ametoa thibitisho hilo katika hali ambayo, Mjumbe Maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran, Brian Hook amesema kuwa, Washington haina mpango wa kuzipa ruhusa nchi zinazonunua mafuta kutoka Iran kufanya hivyo.
Amedai kuwa, nchi tatu kati ya nane ambazo Marekani ilikuwa imeziruhusu ziendelee kununua mafuta ya Iran licha ya vikwazo vya mafuta zimesitisha kikamilifu uagizaji wa mafuta kutoka Iran.
Mnamo Mei 2018, Marekani ilichukua uamuzi wa upande moja wa kujiondoa katika mapatano ya kimataifa ya JCPOA, hatua ambayo imeendelea kukosolewa vikali kimataifa na kupelekea watawala wa Washington kuzidi kutengwa.