Rais Rouhani: Ushirikiano wa Iran na Iraq utastawi zaidi
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amehimiza kustawishwa zaidi uhusiano wa nchi yake na Iraq katika pande zote.
Rais Rouhani amesema hayo leo katika mazungumzo na waandishi wa habari aliyofanya kwa pamoja na Waziri Mkuu wa Iraq, Adil Abdul Mahdi hapa Tehran na huku akibainisha kwamba uhusiano wa mataifa haya mawili ni mkubwa na ni wa kihistoria amesema kuwa, katika kipindi cha karne zote zilizopita, mataifa mawili ya Iran na Iraq yamekuwa na uhusiano mzuri muda wote na kwamba hivi sasa pia uhusiano huo unazidi kuimarika na kustawi.
Aidha amesema, kuna udharura wa kutekelezwa vipengee vya makubaliano yote yanayofikiwa baina ya Tehran na Baghdad na kuongeza kuwa, Iran na Iraq zimetia nia ya kuongeza kiwango cha mabadilishano yao ya kibiashara na kukifikisha kwenye dola bilioni 20 kwa mwaka.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, ushirikiano wa mpakani wa Iran na Iraq katika kupambana na ugaidi, madawa ya kulevya na magendo baina nchi hizi mbili utazidi kuwa mkubwa.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Iraq, Adil Abdul Mahdi al Muntafiki amesema mbele ya waandishi hao wa habari kwamba Iran imeisaidia mno Iraq katika vita dhidi ya ugaidi. Ameongeza kuwa, Iran ina utamaduni na ustaarabu ambao umepenya mno katika historia.
Vile vile amesema, Iraq ina nia ya kweli ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na Iran licha ya kukabiliwa na mashinikizo na vitisho kutoka kwa baadhi ya madola duniani.