Huduma ya Iran kwa wakimbizi; kigezo bora cha kuigwa duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i52811-huduma_ya_iran_kwa_wakimbizi_kigezo_bora_cha_kuigwa_duniani
Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa UNHCR akiwa safarini katika mji wa Mashhad nchini Iran amesema: "Sera za Iran za kuwahudumia wakimbizi na kuhakikisha kuwa hawana matatizo ya kimaisha na wanapata huduma za afya na elimu ni mfano wa kuigwa duniani kote"
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Apr 12, 2019 20:47 UTC
  • Huduma ya Iran kwa wakimbizi; kigezo bora cha kuigwa duniani

Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa UNHCR akiwa safarini katika mji wa Mashhad nchini Iran amesema: "Sera za Iran za kuwahudumia wakimbizi na kuhakikisha kuwa hawana matatizo ya kimaisha na wanapata huduma za afya na elimu ni mfano wa kuigwa duniani kote"

Mulugeta Zewdie ameyasema hayo baada ya kutembelea eneo la Dogharoon katika mkoa wa Khorassan Razavi, kaskazini mashariki mwa Iran ambapo ameishukuru kwa dhati Iran kutokana na huduma ambazo imekuwa ikitoa kwa wakimbizi katika kipindi cha miaka 40 iliyopita. Ameongeza kuwa: "Mbali na kutoa huduma nzuri za mwenyeji kwa wakimbizi, serikali ya Iran imewapa wakimbizi fursa ya kujiimarisha kama raia wa kigeni katika jamii."

Iran inazingatia maadili mema na mafundisho ya Kiislamu na hivyo haitafautishi baina ya wanadamu na kwa msingi huo imekuwa mwenyeji mzuri wa wakimbizi hasa wale ambao wametoka Afghanistan . Kwa muda wa miongo minne sasa, Iran imekuwa mwenyeji wa wakimbizi kutoka nchi mbali mbali ambapo wahajiri kutoka Afghanistan ndio wengi zaidi kutokana na vita vya muda mrefu katika nchi yao.

Wakimbizi wanaofika Iran hawapati tu hifadhi ya kawaida na usalama, bali wakimbizi hao hasa wale wa Afghanistan wanapata fursa za masomo ya msingi, sekondari na vyuo vikuu na pia wanapata huduma kamili za afya. Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kuwa, huduma hizo hawapati tu wakimbizi walioingia nchini na kupata vibali vya kisheria bali hata wale ambao wako Iran kinyume cha sheria wanapata huduma hizo za wakimbizi.

Mulugeta Zewdie

Mwaka 2015, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei, alisema hivi kuhusu haki ya kupata elimu watoto wakimbizi kutoka Afghanistan hata wale ambao wako nchini kinyume cha sheria: "Mtoto Muafghani, hata yule ambaye yuko Iran kinyume cha sheria na bila nyaraka zozote, hapaswi kunyimwa fursa ya kujiendeleza kimasomo na wote wanapaswa kusajiliwa katika shule za Iran."

Agizo hilo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu ulazima wa watoto wote Waafghani nchini Iran kupata masomo katika shule za serikali ni kati ya sera bora zaidi za kuwahudumia wakimbizi na sera kama hivyo ni ya aina yake na ya kipekee duniani. Sera za Iran kuhusu wakimbizi Waafghani ni mfano wa kuigwa duniani kote na  kwa mara kadhaa sasa Umoja wa Mataifa na taasisi husika za umoja huo zimekuwa zikiipongeza Iran kwa ajili ya huduma zake nzuri kwa wakimbizi.

Kuwepo wakimbizi bila shaka ni mzigo mkubwa wa kifedha kwa serikali ya Iran, na kwa kuzingatia huduma ziada ambazo Iran inawapa wakimbizi kutoka Afghanistan, mzigo huo wa kifedha unaongezeka maradufu. Kwa hivyo ni dharura kwa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR kuisaidia serikali ya Iran katika huduma kwa wakimbizi.

Kuhusiana na hili, Abdolreza Rahmani Fazlim Waziri wa Mamboo ya Ndani wa Iran ameashiria kuwepo karibu wakimbizi milioni tatu nchini Iran wakiwemo wenye vibali na wasiokuwa na vibali na kusema: "Iran ina mzigo mzito wa kifedha wa kuwahudumia wakimbizi kwani huwa wanapata huduma na suhula zote zikiwemo za elimu, afya na matibabu na pia makazi."

Wakuu wa Umoja wa Mataifa wanasema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa huduma zaidi ya zile inazotakiwa kwa wakimbizi na inawaunga mkono kikamilifu. Kwa kuzingatia hayo, inatazamiwa kuwa, taasisi husika za kimataifa katika uga wa wakimbizi ziipe Iran misaada zaidi. Hivi sasa UNHCR inatoa mchango mdogo sana katika kuwahudumiwa wakimbizi walioko Iran.

Pamoja na hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuzingatia mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu hasa haki za binadamu za Kiislamu, imefungua milango ya shule, vyuo vikuu na hospitali zake kwa wakimbizi. Hivi sasa wakimbizi kutoka Afghanistan wanapata huduma sawa na Wairani katika sekta mbali mbali. Ni kwa sababu hii ndio wakimbizi Waafghani wameweza kustawi na kufanikiwa wakiwa Iran na hivyo wakataporejea Afghanistan wataweza kuwa na nafasi muhimu katika ustawi wa nchi yao.