Rouhani: Mafuriko ya Iran yamefichua 'hulka chafu' ya watawala wa Marekani
(last modified Wed, 17 Apr 2019 13:49:45 GMT )
Apr 17, 2019 13:49 UTC
  • Rouhani: Mafuriko ya Iran yamefichua 'hulka chafu' ya watawala wa Marekani

Rais Hassan Rouhani ameashiria hatua ya Marekani ya kuzuia kutumwa misaada ya nchi nyingine kwa ajili ya wahanga wa mafuriko hapa nchini Iran, akisisitiza kuwa kitendo hicho kwa mara nyingine tena kimedhihirisha hulka chafu ya watawala wa Washington.

Rais Rouhani ameyasema hayo leo Jumatano katika hotuba yake kwa Baraza la Mawaziri na kubainisha kuwa, Marekani ambayo inajinadi kuwa mtetezi mkuu wa haki za binadamu duniani, imejikuta katika mtihani mkubwa wa kihistoria na kuanika namna isivyokuwa na utu na ubinadamu, kwa kuzuia ufikashaji wa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya waathiriwa wa mafuriko nchini.

Amesema serikali ya Washington sio tu ilikataa kulisaidia taifa la Iran katika janga hilo, bali ilienda mbali zaidi na hata kuizuia jamii ya kimataifa kuwasaidia waathiriwa wa mafuriko, kutokana na vikwazo vyake.

Baada ya kutokea janga hilo la kimaumbile, Marekani ilichukua hatua ya kuzifunga akaunti za fedha zenye mfungamano na Shirika la Hilali Nyekundu la Iran ili kuvuruga shughuli za ufikishaji misaada za shirika la Msalaba Mwekundu na nchi zingine duniani kwa ajili ya watu walioathirika na mafuriko hapa nchini. 

Athari za mafuriko mkoani Khuzestan 

Dakta Rouhani amebainisha kuwa, "Mafuriko yalikuwa mtihani wa kimaanawi kwa taifa hili na Wairani wameweza kuvuta salama na kuupasi mtihani huo. Wairani wameonesha ushirikiano mkubwa baina yao na viongozi wao katika kipindi hicho kigumu cha mafuriko."

Mvua ambazo zimekuwa zikinyesha katika maeneo ya kaskazini, magharibi na kusini mwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimesababisha hasara nyingi za kifedha na kiroho; na kwa mujibu wa idara ya afya nchini Iran jumla ya watu 77 wamepoteza maisha yao katika matukio hayo.