Iran yalaani hujuma za kigaidi nchini Sri Lanka
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i53003-iran_yalaani_hujuma_za_kigaidi_nchini_sri_lanka
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani vikali hujuma za kigaidi nchini Sri Lanka siku ya Jumapili na kusema serikali na watu wa Iran wanafungamna na familia za waathirika wa hujuma hizo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 22, 2019 01:35 UTC
  • Iran yalaani hujuma za kigaidi nchini Sri Lanka

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani vikali hujuma za kigaidi nchini Sri Lanka siku ya Jumapili na kusema serikali na watu wa Iran wanafungamna na familia za waathirika wa hujuma hizo.

Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter, Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameandika: "Nimesikitishwa na hujuma za kigaidi nchini Sri Lanka ambazo zimewalenga waumini wakati wa Pasaka. Tunatuma salamu za rambirambi kwa serikali rafiki na watu wa Sri Lanka. Aidha Zarif ameendelea kuandika kuwa: "Ugaidi ni hatari kwa dunia nzima na wala hauna dini na hivyo walimwengu wote wanapapswa kushirikiana kukabiliana nao."

Kwa upande wake, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Sayyid Abbas Mousavi amelaani vikali mashambulio hayo ya kigaidi nchini Sri  Lanka na kusema: "Jinai hiyo kwa mara nyingine imeonyesha kuwa, ugaidi ni tatizo la dunia lisilo na mipaka na wala halifungamani na kaumu, rangi, taifa au dini." Mousavi ameongeza kuwa: "Ugaidi hauwezi kutokomezwa isipokuwa kwa kuwepo irada imara ya nchi zote na kwa kutumia uwezo wao wote pasina kuwepo sera za undumakuwili."

Katika mawimbi ya mashambulizi ya kigaidi nchini Sri Lanka siku ya Jumapili, watu zaidi ya 207 wameauwa wakati magaidi walipolipua mabomu katika maeneo manane tofauti yakiwemo makanisa matatu na mahoteli manne ya kifahari katika mji mkuu Colombo na miji ya karibu. Kundi la kigaidi la ISIS limedai kuhusika na hujuma hiyo.