Zarif: Iran ina Shahada ya Uzamivu (PhD) ya kukabiliana na vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i53077-zarif_iran_ina_shahada_ya_uzamivu_(phd)_ya_kukabiliana_na_vikwazo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif amesema Jamhuri ya Kiislamu haitasimamisha uuzaji wa mafuta yake nje ya nchi licha ya vikwazo vipya vya Marekani, na kusisitiza kuwa taifa hili lina Shahada ya Uzamivu (PhD) katika kupambana na vikwazo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 25, 2019 03:19 UTC
  • Zarif: Iran ina Shahada ya Uzamivu (PhD) ya kukabiliana na vikwazo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif amesema Jamhuri ya Kiislamu haitasimamisha uuzaji wa mafuta yake nje ya nchi licha ya vikwazo vipya vya Marekani, na kusisitiza kuwa taifa hili lina Shahada ya Uzamivu (PhD) katika kupambana na vikwazo.

Dakta Zarif ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Reuters na kubainisha kuwa, vikwazo vya Washington vinalenga kuwahujuma wananchi wa taifa hili moja kwa moja, lakini serikali itafanya kila iwezalo kuvikwepa vikwazo hivyo.

Katika mahojiano hayo na Reuters mjini New York, Zarif amefafanua kwa kusema, "Bila shaka kuna njia nyingi za kuvizunguka vikwazo. Tuna PhD katika uwanja huo."

Mapema wiki hii, Ikulu ya Marekani (White House) ilitangaza kuwa, nchi nane ambazo zilikuwa zimeruhusiwa na Washington kuendelea kununua mafuta ya Iran licha ya vikwazo vya US ziache kuagiza bidhaa hiyo kuanzia Mei Mosi, vinginevyo zitawekewa vikwazo.

Sekta ya mafuta ya Iran

Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa, hakuna mtu anayeweza kuzuia uuzaji wa mafuta yake nje ya nchi, huku China, Uturuki na baadhi ya wateja wengine wakubwa wa mafuta ya Iran wakipinga vikwazo hivyo vya Marekani.

Kuhusu kitendo cha Marekani cha kuliweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) katika orodha ya makundi yake ya kigaidi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, "Iran haina mpango wa kutoa jibu la kijeshi dhidi ya hatua hiyo ya kipuuzi, lakini iwapo Marekani itabadili kanuni na sheria za maingiliano, Iran haitasita kutoa jibu mwafaka."