Rouhani: Umoja wa Wairani utayashinda mashinikizo ya kila upande ya Marekani
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema umoja na mshikamano wa wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu kwa mara nyingine utatoa pigo kwa vikwazo vya kiuchumi na mashinikizo ya kila upande ya Marekani dhidi ya taifa hili.
Rais Rouhani aliyasema hayo katika kikao na kundi la wanaharakati wa kisiasa hapa mjini Tehran hapo jana na kubainisha kuwa, katu taifa la Iran halitasalimu amri mbele ya mashinikizo hayo.
Amesema, "Kukata tamaa sio katika utamaduni wetu na mafundisho ya dini yetu na taifa la Iran katu haliwezi kukatishwa tamaa na mashinikizo ya adui."
Dakta Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakabiliwa na kipindi kigumu hivi sasa ambacho hakijawahi kushuhudiwa tena katika historia, lakini amesisitiza kuwa Wairan watavuka salama changamoto za sasa kutokana na umoja wao na kusimama kwao kidete.
Amefafanua kuwa, "Wakati wa vita (vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran), hatukuwa na matatizo ya kibenki, uuzaji wa mafuta pamoja na uagizaji na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi. Vikwazo vilivyotukabili wakati huo vilikuwa vya silaha tu."
Dakta Rouhani amesema taifa la Iran kamwe haliwezi kujitweza na kujidhalilisha mbele ya Marekani, na bila shaka litayapatia ufumbuzi matatizo yanayolikabili.