Iran yakosoa matamshi ya Rais wa Ufaransa alipokutana na Trump
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu matamshi ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alipokutana na mwenzake wa Marekani mjini Paris na kusema matamshi ya Macron hayasaidii katika kulindwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Katika taarifa, Sayyid Abbas Mousavi, amesema kuwa nchi za Ulaya hadi sasa pamoja na hotuba na taarifa kadhaa, hazijaweza kuchukua hatua za kivitendo kutekeleza ahadi zao katika mapatano ya JCPOA baada ya Marekani kujiondoa kinyume cha sheria katika mapatano hayo. Ameongeza kuwa nchi za Ulaya zimekuwa zikiibua masuala yasiyohusiana na JCPOA jambo ambalo si tu kuwa halisaidii chochote katika kulinda JCPOA bali linaandaaa mazingira ya kuondoa kabisa imani iliyobakia baina ya pande zilizosalia katika mapatano hayo sambamba na kuiwezesha Marekani kufikia mlengo yake yaliyo kinyume cha sheria katika mapatano hayo ya kimataifa. Mousavi ametahadahrisha kuwa jambo hilo yamkini likapelekea mapatano ya JCPOA kuangamia kikamilifu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema madai ya kukaririwa ya Rais wa Marekani katika mkutano na mwenzake wa Ufaransa hayana msingi wala thamani na hakuna haja hata ya kuyajibu.
Rais Macron wa Ufaransa, ambaye nchini yake kama mwanachama wa JCPOA, haijatekeleza mapatano hayo kivitendo, Ijumaa alasiri akiwa katika kikao cha pamoja cha waandishi habari na Rais Donald Trump alisema: "Paris na Washington zinafuatilia lengo la pamoja na mazungumzo mapya yanapaswa kufanyika ili kupanua wigo wa JCPOA."
Katika mkutano, huo Trump alikariri tuhuma zake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kudai kuwa eti 'Iran haipaswi kumiliki silaha za nyuklia.' Matamshi hayo ya Trump yanatolewa katika hali ambayo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki hadi sasa umetoa ripoti 15 zinazoonyesha kuwa mpango wa nyuklia wa Iran ni wa malengo ya amani na kwamba nchi hii inafungamana na ahadi zake katika mapatano ya JCPOA.