Rais Rouhani: Marekani ni tishio kuu kwa uthabiti wa dunia
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani ni tishio kubwa kwa usalama na uthabiti wa nchi za eneo la Asia Magharibi na duniani kote kwa ujumla.
Rais Rouhani amesema hayo leo Ijumaa katika mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai SCO huko Bishkek, mji mkuu wa Kyrgyzstan. Jumuiya hiyo ya kiusalama inazijumuisha nchi mbalimbali za eneo la Eurasia kama vile China, Russia na India.
Dakta Rouhani amebainisha kuwa, "Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, serikali ya Marekani imekuwa ikitumia uwezo wake wa kiuchumi, kifedha na kijeshi na kwa njia za mabavu kuvuruga mifumo na kanuni za kimataifa."
Rais wa Iran ameeleza bayana kuwa, ubeberu huo wa Marekani umeigeuza nchi hiyo na kuwa tishio kubwa zaidi kwa uthabiti wa eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) na kimataifa.
Amesisitiza kuwa, "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaitakidi kwamba, hii leo jamii ya kimataifa inakabiliwa na changamoto kubwa wakati huu kuliko wakati wowote mwingine ule, kutokana na sera za kibeberu. Matatizo yanayoukumba ulimwengu wa leo kama vile ugaidi, misimamo ya kuchupa mipaka na ulanguzi wa mihadarati yanafanya sera ya uhusiano wa pande kadhaa kuwa jambo la dharura."
Rais wa Iran ameongeza kuwa, nchi za dunia kuanzia mashariki hadi magharibi zinapaswa kuwa na ushirikiano na umoja, kwa lengo la kuyatokomeza matatizo ya ugaidi na uchupaji mipaka ambao unatishia amani, uthabiti na maendeleo ya dunia.