Zarif: Wamarekani wametengwa katika siasa za kimataifa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezitaja siasa na machaguo yasiyofaa ya Marekani kuwa miongoni mwa sababu za ushindi wa muqawama na kutengwa Washington katika uga wa siasa za kimataifa.
Muhammad Javad Zarif amesema kuwa Wamarekani wanadhani kuwa kwa kutumia wenzo wa vikwazo wataweza kuangamiza uchumi wa Iran na kuongeza kuwa: Taifa la Iran limebatilisha mahesabu yote ya Wamagharibi, Wamarekani na wale wote wanaoitakia mabaya Iran kwa kutegemea uwezo wa wananchi.
Zarif amesisitiza kuwa siasa za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na ulimwenguni kwa ujumla zitafeli na kushindwa na kueleza kuwa: Marekani inafanya ugaidi wa kiuchumi baada ya kushindwa siasa zake kieneo na kimataifa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, Marekani jana usiku iliitisha kikao maalumu cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) hata hivyo ilishindwa hata kupata taarifa fupi tu iliyo dhidi ya Iran kutoka kwa Mwenyekiti wa bodi hiyo.
Ameongeza kusema kuwa tangu mwaka jana Marekani imekwishaitisha mara nne vikao vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambavyo baadhi vilihudhuriwa na Rais wa nchi hiiyo lakini Wamarekani hawakufanikiwa kuwashawishi hadhirina kutoa matamshi ya aina yoyote dhidi ya Iran.
Kikao cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) kilifanyika jana alasiri huko Vienna Austria makao makuu ya wakala wa IAEA kufuatia ombi la Marekani. Marekani ilitaka kufanyika kikao hicho cha dharura ili kuchunguza hatua za karibuni za Iran za kupunguza ahadi na majukumu yake kuhusiana na makubaliano ya JCPOA.
Kadhim Gharib-Abadi Balozi wa Kudumu wa Iran katika Taasisi za Kimataifa zenye makao yake mjini Vienna amesema kuwa kikao maalumu cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa IAEA kimemalizika bila ya matunda yoyote kwa Marekani.