Uturuki yaihakikishia Iran, mashambulizi yake Syria ni ya muda mfupi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56490-uturuki_yaihakikishia_iran_mashambulizi_yake_syria_ni_ya_muda_mfupi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amemhakikishia mwenzake wa Iran kwamba, mashambulizi ya jeshi la nchi hiyo huko kaskazini mwa Syria yaliyoanza Jumatatu usiku ni ya muda mfupi.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Oct 08, 2019 04:53 UTC
  • Uturuki yaihakikishia Iran, mashambulizi yake Syria ni ya muda mfupi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amemhakikishia mwenzake wa Iran kwamba, mashambulizi ya jeshi la nchi hiyo huko kaskazini mwa Syria yaliyoanza Jumatatu usiku ni ya muda mfupi.

Mevlut Cavusoglu amesema hayo katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Iran Muhammad Javad Zarif huku jeshi la Uturuki likianza operesheni ya kuwasaka waasi wa Kikurdi huko kaskazini mwa Syria.

Duru za maeneo hayo zimeripoti kuwa, jeshi la Uturuki limeanza kushambulia ngome na vituo vya kundi la People's Protection Units (YPG) la Wakurdi wa Syria katika mji wa al-Malikiyah ambalo serikali ya Ankara inadai lina mfungamano na magaidi wa kundi la PKK.

Katika mazungumzo hayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ametilia mkazo udharura wa kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala ya Syria akisisitiza kuwa mashambulizi ya nchi yake kaskazini mwa Syria ni ya muda mfupi.

Jeshi la Uturuki huko kaskazini mwa Syria 

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza upinzani wa Tehran dhidi ya harakati zote za kijeshi na kuitaka Uturuki iheshimu ardhi na mamlaka ya Syria.

Muhammad Javad Zarif pia ametilia mkazo udharura wa kupambana na ugaidi huko Syria kwa ajili ya kurejesha amani na usalama nchini humo. Hata hivyo amesema makubaliano ya Adana ndiyo wenzo bora zaidi wa pande mbili za Syria na Uturuki kwa ajili ya kutatua matatizo yao.

Makubaliano ya Adana ya Kupambana na Ugaidi yalitiwa saini na Uturuki na Syria tarehe 20 Oktoba mwaka 1998.