Kamanda Fadavi: Akthari ya wafanya ghasia, walitiwa mbaroni wakijaribu kutoroka Iran
Kaimu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, Ali Fadavi amesema kuwa akthari ya wafanya ghasia za hivi kariuni walitiwa mbaroni wakati wakijaribu kutoroka Iran.
Jenerali Fadavi aliyasema hayo jana Jumatano ambapo sambamba na kubainisha kwamba akthari ya wafanya ghasia za hivi karibuni nchini Iran, waliwahi kuwa na kesi na mafaili tofauti ya jinai, ameongeza kuwa kwa kuzingatia kuwa wafanya ghasia hao walifahamu kuwa wametenda jinai na kumwaga damu za watu, walijaribu kutoroka nchi, lakini wakatiwa mbaroni na vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amezidi kufafanua kuwa, kutokana na weledi wa hali ya juu raia wa Iran walisimama safu moja na kujitenga na wafanya ghasia. Amesema wananchi wa Iran wanafahamu vyema ukhabithi wa maadui ambapo kama ilivyokuwa katika kipindi cha miongo minne iliyopita, kwa mara nyingine tena wamesambaratisha njama za maadui.
Itakumbukwa kuwa, hatua ya kuifanyia marekebisho bei ya mafuta ya petroli nchini Iran hapo Novemba 15 mwaka huu, ilipelekea kuibuka maandamano ya amani ya wananchi mjini Tehran na baadhi ya miji mingine ya nchi. Hata hivyo kundi fulani la wafanya ghasia na ambalo lilipewa mafunzo na maadui wa Iran, lilijipenya katika maandamano hayo na kuanza kuharibu mali za umma na za watu binafsi zikiwemo benki, idara, magari ya kubeba wagonjwa na magari ya usafiri. Kufuatia uharibifu huo, wananchi wa Iran katika miji mbalimbali walifanya maandamano makubwa na ya hamasa ambapo sambamba na kutangaza kujitenga mbali na wafanya ghasia hao vibaraka, waliunga mkono usalama na izza ya taifa hili.