Iran yalaani vikali matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali matamshi yalivyo dhidi ya Iran ya Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani na kusema: "Udiplomasia na sera za kigeni za Marekani zimefeli, zimejaa ndoto, zimedumaa na ni za mabavu."
Siku ya Alkhamisi, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani alitoa madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran na kuituhumi nchi hii kuwa inakiuka haki za binadamu.
Katika kujibu matamshi hayo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Sayyid Abbas Mousavi amesema Ijumaa kuwa, Pompeo amekuja katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani baada ya kuwa msimamizi ya shirika la kijahanamu (la CIA), lenye hadaa, la kutesa watu na kupindua serikali zingine. Amesema hivi sasa Pompeo ameleta fikra zake hizo za kijahanamu katika medani ya kidiplomasia. Ikumbukwe kuwa kabla ya kuwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani, Pompeo alikuwa mkuu wa Shirika Kuu la Kijasusi la Marekani, CIA.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa utendaji kazi wa Pompeo si wa hadhi ya waziri wa mambo ya nje katika uga wa kimataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameendelea kusema kuwa, mawaziri wa mambo ya nje kwa kawaida huwa ni wenye kunadi amani, maelewano, mazungumzo na kuheshimiana lakini Pompeo anapigia debe utumiaji mabavu, hadaa, udhalilishaji,uvunjiaji heshima, lugha ya vitisho, ujahili, ujinga na uafiriti.
Aidha Mousavi amesema kuwa, Wamarekani hawatafika popote kwa mbinu zao hizo.