Rais Rouhani: Mashinikizo ya kiuchumi ya Marekani hayalilengi taifa la Iran pekee
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mashinikizo ya kiuchumi ya Marekani hayalilengi taifa la Iran pekee, bali kuna mataifa mengine ya dunia ambayo nayo yanaandamwa na siasa hizi za Washington za kuzishinikiza kiuchumi nchi nyingine.
Akizungumza leo katika kikao na baraza lake la mawaziri Rais Rouhani ametoa pia mkono wa kheri na pongezi kwa Wakristo wote ulimwenguni kwa sikukuu yao ya Krismasi na kuzaliwa Nabii Issa Masihi (as) inayoadhimishwa leo na kueleza kuwa, Issa ni mmoja wa Mitume wakubwa wa Mwenyezi Mungu.
Akizungumzia vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi ya Marekani dhidi ya Iran, Rais Rouhani amesema kuwa, siyo Iran pekee ambaye leo inaandamwa na vikwazo hivyo vya Washington.
Rais wa Iran amesema pia kuwa, hii leo nchi zote yakiwemo mataifa yaliyoshiriki hivi karibuni katika "Mkutano wa Kual Lumpur 2019" yanashinikizwa na Marekani ambayo inayaona mataifa hayo kuwa yanakwamisha mashinikizo ya White House dhidi ya Tehran.
Matatizo ambayo leo wananchi wa Iran wanakabiliwa nayo kutokana na mashinikizo ya kiuchumi ya serikali ya Marekani, mataifa mengine ya dunia pia nayo yanakabiliwa na matatizo haya, amesisitiza Rais Rouhani.
Kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Rais Rouhani amesema kuwa, kundi la 5+1 litaonyesha nia njema na irada ya kutaka kutekeleza ahadi zao zote za huko nyuma, basi Iran iko tayari kufanya mazungumzo.
Kadhalika amesema kuwa, hii leo kama mnaona katika maeneo mbalimbali ya dunia Iran inaheshimika na maneno yake yana soko, basi hilo linatokana na kusimama kidete taifa hili na kutokubali kuburuzwa au kudunishwa.