Rouhani: Tumepata njia mpya za kufanya biashara na nchi mbalimbali
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa leo hii Iran imepata njia mpya za kufanya biashara na nchi mbalimbali za dunia na kwamba imepiga hatua mpya katika uwanja huo na nchi kama India, Malaysia, Uturuki, China na Russia.
Rais Hassan Rouhani amebainisha kuwa katika kikao cha pande nne kati ya Iran, Malaysia, Uturuki na Qatar kulikuwa na mitazamo ya pamoja kuhusu masuala ya kibenki na fedha; na kusisitiza kuwa nchi za ulimwengu zinapasa kuachana na matumizi ya sarafu ya dola.
Rais wa Iran amesema kuwa hii leo nchi mbalimbali duniani zikiwemo nchi zilizoshiriki katika mkutano wa karibuni huko Malaysia zinafahamu vyema kuwa Marekani ndio mkosa katika kuliweka chini ya mashinikizo taifa la Iran. Amesema, hakuna aliye na shaka kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza kikamilifu majukumu yake na kuchukua hatua chanya kuhusiana na masuala ya amani, uthabiti na usalama wa kieneo na kimataifa na kwamba ni upande wa pili ndio umepuuza majukumu yake.
Rais Rouhani ameongeza kuwa sisi tupo tayari kufanya mazungumzo iwapo nchi za kundi la 5+1 leo hii zitakuwa na azma ya kutekeleza majukumu yao yote na kufidia makosa yao ya huko nyuma.