Jan 19, 2020 08:04 UTC
  • Iran yasema ikilazimu, itaangalia upya ushirikiano wake na IAEA

Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amezionya nchi za Ulaya kuwa, Tehran italazimika kuangalia upya ushirikiano wake na Wakala wa Kimataifa wa Niashati ya Atomiki (IAEA) iwapo EU itaendelea kuchukua hatua zisizo za kiadilifu juu ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Indhari hiyo ya Dakta Ali Larijani imetolewa baada ya Troika ya Ulaya, yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuanzisha mchakato wa kutatua hitilafu ndani ya JCPOA unaofahamika kama 'Trigger Mechanism' kwa kisingizio kuwa Iran haifungamani na wajibu na majukumu yake kwenye mapatano hayo.

Akizungumza katika kikao cha Bunge hii leo, Spika Larijani amesema, "hatua hiyo ya Ulaya haina mfungamano wowote na hatua zilizochukuliwa na Iran, bali imetokana na mashinikizo ya Marekani."

Spika wa Bunge la Iran ameeleza bayana kuwa, ni jambo la kusikitisha kwa waziri mmoja wa mambo ya nje wa Ulaya kukiri wazi wazi kuwa, walichukua hatua hiyo baada ya kutishiwa na Trump kuwa atayawekea ushuru mpya wa asilimia 25 magari yanayotoka nchi hizo za Ulaya. 

Wakuu wa Troika ya Ulaya wanaoshinikizwa na Trump

Licha ya kutumbukia kwenye mashinikizo hayo ya Trump na kutaka kufanyika mazungumzo mapya ya nyuklia, lakini nchi hizo za Ulaya zinadai kuwa haziungi mkono sera ya Washington ya kuiwekea Iran mashinikizo ya hali ya juu.

Baada ya nchi za Ulaya kushindwa kudhamini maslahi ya Iran kwenye makubaliano hayo baada ya Marekani kujiondoa, Iran iliamua kuchukua hatua kwa awamu tano za kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA.

 

Tags