May 17, 2020 06:47 UTC
  • Ombi la Umoja wa Mataifa kuhusu kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran

Baada ya serikali ya Rais Donald Trump kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) mwaka 2018 katika fremu ya sera za mashinikizo ya juu kabisa na kisha kushadidisha vikwazo ambavyo havijawahi kushuhudiwa katika historia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na licha ya kuibuka ugonjwa wa COVID-19 nchini Iran, lakini bado Trump anasisitiza kuendeleza vikwazo vyake vilivyo dhidi ya ubinadamu dhidi ya taifa hili.

Vikwazo hivyo vya Trump vinakosolewa sana kimataifa na kumetolewa maombi kadhaa ya kutaka vikwazo hivyo vya kidhalimu dhidi ya Iran viondolewe. Ombi la hivi karibuni kabisa limetolewa na Michelle Bachelet Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa  ambaye Ijumaa kwa mara nyingine alisisitiza udharura wa kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran ili kuisaidia nchi hii ipambane ipaswavyo na janga la COVID-19.

Katika mahojiano, Bachelet amesema: "Katika hali ya hivi sasa vikwazo vyote vya Marekani dhidi ya Iran na Venezuela vinapaswa kuondolewa ili kuokoa maisha ya wanadamu. Hatua zilizochukuliwa na serikali ya Trump katika kuondoa vizingiti vya kuuzwa vifaa vya tiba ambavyo vimewekewa vikwazo ni dhaifu sana  na hivyo kuondolewa au kusimamishwa kwa muda vikwazo ndilo jambo tu linaloweza kuwa na taathira inayokusudiwa.

Baada ya kuenea ugonjwa wa COVID-19, serikali ya Trump imeombwa mara kadhaa kuondoa au kusimamisha kwa muda vikwazo dhidi ya Iran lakini wakuu wa Washington wamepuuza kabisa maombi hayo ya jamii ya kimataifa.

Washington inadai bidhaa za kibinaadamu na kitiba zimeondolewa vikwazo lakini wataalamu wanasema, vikwazo vya kibenki dhidi ya Iran vimepelekea mashirika mengi yasiwe na hamu ya kufanya biashara na Iran.

Ukweli ni kuwa, mashirika mengi na hata nchi nyingi zinajiepusha kuisaidia au kushirikiana na Iran kwa kuhofia adhabu ya Marekani. Kwa msingi huo ili kuzuia kujiingiza katika matatizo, mashirika mengi yanajizuia kufanya biashara na Iran hata katika uga wa vifaa vya tiba na dawa.

Serikali ya Trump  awali ilikuwa inadai kuwa, kwa kuzingatia masuala ya haki za binaadamu itaondoa baadhi ya vikwazo dhaifu dhidi  ya Iran lakini haijachukua hatua zozote za kivitendo kuhusu suala hilo.

Wakati huo huo vikwazo vilivyo dhidi ya binadamu vya Washington havijaweza kufanikiwa kuilazimisha Iran kusalimu amri na kutii matakwa yasiyo ya kisheria ya Marekani. Kutokana na hali hiyo, Trump sasa ameingiwa na hasira na ametoa amri ya ugaidi wa kiuchumi na kushadidisha hatua zilizo dhidi ya ubinadamu dhidi ya watu wa Iran. Kati ya hatua ambazo Trump amezichukua ni kuiwekea Iran vizingiti kadhaa katika ununuzi wa dawa na bidhaa za kimsingi kutoka nchi zingine. Kadhia hii katika kipindi hiki cha janga la COVID-19 imepelekea kuibuka changamoto kubwa katika mfumo wa afya na matibabu nchini Iran. Pamoja na kuwepo hali mbaya ya hivi sasa, wakuu wa utawala wa Trump wangali wanasisitiza kuendeleza mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran.

Brian Hook, mwakilishi maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran katika mahojiano ya tarehe 26 Aprili alikariri baadhi ya madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran na kusema eti sera za mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran zimefanikiwa.

Kinyume na madai hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama kidete dhidi ya mashinikizo hayo yote yasiyo na kifani ya Marekani ambayo yanatekelezwa ili kuilazimisha Tehran itekeleze matakwa yasiyo ya kisheria ya Washington. Kwa msingi huo sera za utawala wa Trump dhidi ya Iran zimegonga mwamba.

Rais Trump

Katika upande mwingine, kila siku kunashuhudiwa kuongezeka miito ya kutaka kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran. Hivi sasa mbali na washirika wa Iran kimataifa, hata waitifaki wa Marekani nao pia wanataka vikwazo dhidi ya Iran viondolewe. Hivi karibuni kundi la wabunge wa Bunge la Ulaya mnamo Mei 13 walimuandikia barua Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya Josep Borrell na  Charles Michel Mkuu wa Baraza la Ulaya ambapo wametaka vikwazo dhidi ya Iran na nchi zingine zote viondolewe katika wakati huu wa janga la COVID-19.

Lakini pamoja na hayo,  Marekani imekaidi matakwa hayo ya kibinaadamu ya jamii ya kimataifa. Katika fremu hii, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani mwishoni mwa mwezi Aprili 2020 ilitoa taarifa na  kupuuzilia mbali kampeni ya kutaka vikwazo dhidi ya Iran viondolewe na kusisitiza kuwa  vikwazo  hivyo vitaendelea.

Kama alivyosema Jamal Zahran, mhadhiri wa uhusiano wa kimataifa, kuendelea vikwazo dhidi ya Iran katika mazingira ya COVID-19 ni jinai dhidi ya binadamu.

 

 

Tags