Rais Rouhani: Waislamu wasimame kidete kutetea na kulinda thamani za Uislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i63349-rais_rouhani_waislamu_wasimame_kidete_kutetea_na_kulinda_thamani_za_uislamu
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kulaani kitendo cha jarida la Charlie Hebdo la Ufaransa cha kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW, ameyataka mataifa ya Kiislamu kusimama kidete kutetea na kulinda thamani, utamaduni na matukufu ya dini yao.
(last modified 2025-11-16T06:33:27+00:00 )
Sep 11, 2020 04:46 UTC
  • Rais Rouhani: Waislamu wasimame kidete kutetea na kulinda thamani za Uislamu

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kulaani kitendo cha jarida la Charlie Hebdo la Ufaransa cha kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW, ameyataka mataifa ya Kiislamu kusimama kidete kutetea na kulinda thamani, utamaduni na matukufu ya dini yao.

Rais Rouhani alitoa mwito huo jana Alkhamisi na kubainisha kuwa, Wazayuni ndio waliohusika na kitendo hicho kilichochoma nyoyo za Waislamu kote duniani. Ameeleza bayana kuwa, "Wazayuni na vibaraka wao kwa mara nyingine wamefungua mlango wa kutukanwa na kuvunjiwa heshima Uislamu na Mtume Muhammad SAW."

Dakta Rouhani amesisitiza kuwa, dunia hivi sasa ipo katika kipindi nyeti na hasasi sana na ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kutetea thamani za dini yao kwa nguvu zote.

Kadhalika Rais Rouhani amewapongeza wananchi Waislamu wa Iran kwa kupaza sauti zao kulaani vitendo vya kuvunjiwa heshima Uislamu na matukufu yake, kama vile kitendo hicho cha kuvunjiwa heshima Mtume Mtukufu SAW, njama iliyopikwa na Wazayuni; dhulma dhidi ya wananchi wa Palestina; na vitendo vingine vya kinafiki dhidi ya utamaduni wa Kiislamu.

Maandamano ya Wairani ya kulaani kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW huko Ufaransa

Jana Alkhamisi, wananchi wa Iran katika kona zote za nchi waliandamana kulaani kwa nguvu zao zote ufidhuli wa jarida ya Charlie Hebdo la Ufaransa wa kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW na pia kitendo cha maadui wa Uslamu cha kuchoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu katika mji wa Malmö wa kusini mwa Sweden.

Aidha Jumanne iliyopita, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alilaani vikali hatua ya jarida la Ufaransa la Charlie Hebdo ya kuchapisha tena vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (SAW) na kusisitiza kuwa: Njama hizo za Marekani na utawala wa Kizayuni ni dhambi isiyosameheka.