Wananchi wa Iran washiriki duru ya pili ya uchaguzi wa Bunge
Wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameelekea katika masanduku ya kupigia kura kushiriki duru ya pili ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran).
Wananchi wa Iran sambamba na kuchunga protokali za afya katika kipindi hiki cha janga la corona, wanatazamiwa kuwachagua wabunge wao katika maeneobunge 10 katika uchaguzi huu.
Wapigakura na maafisa wote wanaosimamia shughuli hii ya kidemokrasia wanalazimika kuvalia barakoa na glavu mkononi mbali na kutakiwa kusimama umbali wa mita mbili.
Vituo 3,100 vya kupigia kura katika maeneobunge 10 ya nchi hii vilifunguliwa leo saa mbili asubuhi kwa saa za hapa nchini. Duru ya pili ya uchaguzi wa Bunge la 11 la Iran ilipaswa kufanyika mwezi Machi mwaka huu, lakini ikaakhirishwa kutokana kushika kasi maambukizi ya virusi vya corona. Duru ya kwanza ya uchaguzi huo ilifanyika Februari 21 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran, asilimia 42.57 ya wananchi wa Iran walishiriki katika uchaguzi wa duru ya 11 ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge mwezi Februari mwaka huu. Zaidi ya wagombea elfu saba na 157 walichuana katika majimbo 208 ya uchaguzi kwa ajili ya viti 290 vya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu.
Uchaguzi katika Jamhuri ya kiislamu ya Iran, ni kielelezo cha kushirikishwa wananchi katika kuchukua maamuzi muhimu ya kisiasa na kijamii na zoezi hilo linatambuliwa kuwa ni wajibu wa kisheria na kidini na haki ya kiraia ya kila Muirani.