Iran: Historia haitowasamehe wauaji na wasaliti
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i63744-iran_historia_haitowasamehe_wauaji_na_wasaliti
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuwa, historia haiwezi kamwe kuwasamehe wauaji na wasaliti.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 30, 2020 23:02 UTC
  • Iran: Historia haitowasamehe wauaji na wasaliti

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuwa, historia haiwezi kamwe kuwasamehe wauaji na wasaliti.

Ikitoa taarifa yake kwa mnasaba wa Siku ya Kushikamana na Watoto wa Palestina, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeandika katika ukurasa wake rasmi wa Twitter kwamba; "Miaka 20 nyuma, Muhammad al Durrah aliuliwa kikatili na kinyama mno tena kwa makusudi na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni akiwa pembeni mwa baba yake na hivyo kuwaonesha walimwengu ukatili uliochupa mipaka wa wavamizi wa Quds."

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeongeza kuwa, miaka 20 baada ya ukatili na unyama huo, zimejitokeza tawala za eneo la Asia Magharibi na kuungana na wauaji wa kijana huyo mdogo wa Kipaletina; historia haiwezi kuwasamehe wauaji na wasaliti.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Wiki za hivi karibuni tawala za kiimla za nchi mbili za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Bahrain zilitangaza rasmi kuweka uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao mikono yake imejaa damu za watoto wasio na hatia wa Palestina.

Tarehe 30 Septemba imepewa jina la Siku ya Kushikamana na Watoto wa Palestina katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ili kuubakisha hai unyama aliofanyiwa kijana mdogo wa Kipalestina Muhammad al Durrah na wanajeshi makatili wa utawala wa Kizayuni.

Tarehe 30 Septemba mwaka 2000, katika siku za awali za Intifadha ya Pili yaani Intifadha ya al Aqsa, vyombo vya habari vilirusha hewani picha za kijana wa miaka 12 wa Kipalestina, Muhammad al Durrah, ambaye alikuwa akijificha vilivyo nyuma ya baba yake ili asipigwe risasi na Wazayuni, lakini wanajeshi hao makatili walimpiga risasi kichwani na kumuua shahidi kwa makusudi ili kumuumiza zaidi baba yake na kuonyesha walivyo makatili kupita kiasi.