Hotuba ya Kiongozi Muadhamu katika maadhimisho ya Kubaathiwa Mtume (saw)
Kupambana na harakati ya ujahili, ndilo jukumu muhimu zaidi la Umma wa Kiislamu.
Hayo yamesemwa Leo Alkhamisi na Ayatullah Ali Khamanei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alipokuwa akihutubia umati mkubwa wa viongozi wa Mfumo wa Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu wanaoziwakilisha nchi zao humu nchini na familia za mashahidi katika maadhimisho ya siku ya kubaathiwa na kupewa utume Mtume Mtukufu Muhammad (saw). Huku akisisitiza juu ya jukumu hilo zito na muhimu, Ayatullah Khamanei ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ikiwa ndiyo iliyo kwenye mstari wa mbele na inayoongoza harakati ya mab'ath katika njia iliyoanzishwa na Imam Khomeini (MA), itaendelea mbele na harakati hii bila ya kuyaogopa madola yenye nguvu duniani. Ameashiria mahitaji ya siku zote ya binadamu kwa mafundisho ya mab'ath na kusema kuwa harakati ya ujahili ni mrendo unaokabiliana na mab'ath hiyo. Ameongeza kuwa harakati ya ujahili haihusiani tu na zama za Mtume (saw) bali ni mrengo wa kudumu unaokabiliana na fikra ya wongofu iliyoanzishwa na Mitume, mrengo ambao hii leo umedhihiri katika sura mpya kutokana na matumizi ya elimu na teknolojia ya kisasa.
Sisitizo la Kiongozi Muadhamu la azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo inaoongoza harakati ya mab'ath, ya kuendelea mbele bila kuyaogopa madola yenye nguvu duniani, linakumbusha malengo ambayo Mapinduzi ya Kiislamu yameyafikia na kwa kuendelea mbele kwa kishindo kwenye njia hiyo, yamekuwa yakivunja ngome za ubeberu wa Marekani. Tokea mwanzoni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliweka wazi njia yake na kujitenga na nchi za kidhalimu na kusimama imara mbele ya harakati za kijahili bila kutegemea wala kufungamana na kambi ya Mashariki.
Kwa kuzingatia hilo si ajabu kuiona Marekani na nchi nyingine zinazofungamana nayo zikieneza duniani propaganda kubwa na sumu dhidi ya Uislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ushia. Marekani imeelewa vyema athari ya harakati hii ambayo ni mwamko wa Kiislamu na kuitaja kuwa changamoto kubwa zaidi iliyo mbele ya mfumo wa ubeberu na utawala wa Kizayuni, na hivyo kufanya kila inaloweza ili kuiandalia Israel mazingira ya amani na usalama. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndipo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akasisitiza kuwa harakati ya Kizayuni inayotawala duniani ni mfano wa wazi wa mifumo ya mashetani na kuongeza kuwa hali ya hivi sasa ya dunia inatokana na udhibiti wa mtandao mkubwa wa mabepari wa Kizayuni ambao wamepenya na kuzidhibiti hata serikali kubwa ulimwenguni kama vile ya Marekani.
Hata hivyo, matukio ya miaka kadhaa iliyopita yanaonyesha kwamba utawala haramu wa Israel unakabiliwa na hali ngumu sana na hasa baada ya kudhihiri mwamko wa Kiislamu na kwa hivyo Marekani na waungaji mkono wengine wa utawala huo wa kibaguzi wanafanya kila wanaloweza ili kuharibu umoja wa Waislamu na hivyo kuweka hatarini suala la kudumishwa mapambano ya Kiislamu na umoja wa Umma wa Kiislamu. Jambo linalofuatiliwa kwa karibu na Marekani kuhusiana na suala la kuifanya Iran na Uislamu uogopwe duniani ni kuudhaminia usalama utawala ghasibu wa Israel na kulinda nafasi ya utawala huo haramu kwa kuyadhoofisha makundi ya mapambano ya Kiislamu katika nchi za Syria, Lebanon na Palestina.
Kwa msingi huo hatari kuu inayoukabili ulimwengu wa Kiislamu hii leo, ni kughafilika kuhusiana na misingi na thamani halisi za mwamko wa Kiislamu na pia kughafilika kuhusiana na tishio la Marekani na utawala haramu wa Israel katika eneo la Masharikiya Kati. Katika zama hizi ambazo ni zama za kuamka mataifa yanayodhulumiwa dhidi ya mifumo ya kishetani, nchi za Magharibi zina wasiwasi mkubwa kuhusu mwamko wa Kiislamu na kubaleghe kisiasa mataifa, na kwa hivyo zinatumia mbinu tofauti kufanya Uislamu na Iran ziogopwe duniani na hivyo kutoa picha mbaya, potovu na isiyo ya kweli kuhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbele ya macho ya walimwengu. Pamoja na uchochezi na njama hizo zote za Wamagharibi dhidi ya Iran lakini kufikia sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa pakubwa katika kuyatetea mataifa yanayodhulumiwa na hivyo kuyapa changamoto kubwa madola yenye nguvu duniani. Makabiliano hayo kwa hakika ni vita visivyomalizika dhidi ya madola ya uistikbari na yanayoeneza fikra za zama za ujahili. Ni wazi kuwa madamu kipindi cha dhulma na ujahili kinaendelea mapambano nayo hayatamalizika. Kama alivyosisitiza Ayatullah Khamenei, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haijawahi kuanzisha vita wala harakati ya kijeshi dhidi ya nchi yoyote ile lakini imebainisha na itaendelea kubainisha wazi tena kwa sauti kubwa misimamo yake thabiti.