Waziri wa Ulinzi wa Iraq aonana na Brigedia Jenerali Baqeri
Waziri wa Ulinzi wa Iraq ambaye yuko ziarani hapa nchini Iran ameonana na kuzungumza na Mkuu wa Komandi Kuu ya Vikozi vya Ulinzi vya Iran.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr, Waziri wa Ulinzi wa Iraq, Luteni Jenerali Juma Anad Saadoun, leo ameonana na Brigedia Jenerali Muhammad Baqeri hapa Tehran na kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali yanayozihusu nchi mbili.
Waziri wa Ulinzi wa Iraq amekuja hapa Tehran kwa ajili ya kustawisha uhusiano wa kiulinzi na kijeshi wa pande mbili na kujadiliana na viongozi wa Iran masuala kama ya kupambana na ugaidi, kuimarisha usalama katika eneo hili na kutafuta njia za kupambana na ukosevu wa utulivu katika eneo hili kwa kustafidi vizuri na uzoefu na uwezo wa kiteknolojia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kabla ya hapo, Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Amir Hatami alikuwa amesema kwamba, Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kudhamini mahitaji ya vikosi vya ulinzi vya Iraq kwa shabaha ya kuimarisha uwezo wa kiulinzi wa nchi hiyo. Brigedia Jenerali Amir Hatami alisema hayo jana Jumamosi hapa mjini Tehran katika mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Iraq Luteni Jenerali Juma Anad Saadoun anayeitembelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema, inapasa nchi za eneo zenyewe zidhamini na kushughulikia usalama wa eneo lao na akaongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kuunga mkono mchakato wa kisiasa, uthabiti, usalama na umoja wa ardhi yote ya Iraq kama ilivyokuwa hapo awali na iko tayari kushiriki katika ujenzi mpya na ustawi wa nchi hiyo.