Gharib Abadi: Tutafuatilia kisheria kufichuliwa ripoti ya siri ya IAEA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i65035-gharib_abadi_tutafuatilia_kisheria_kufichuliwa_ripoti_ya_siri_ya_iaea
Mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao Vienna amesema, kuhusu kutangazwa katika chombo kimoja cha habari cha Magharibi ripoti ya siri ya hivi karibuni ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, kwamba karibuni hivi Iran italifuatilia kisheria na kwa uzito mkubwa suala hilo.
(last modified 2026-08-14T10:24:44+00:00 )
Dec 06, 2020 03:53 UTC
  • Gharib Abadi: Tutafuatilia kisheria kufichuliwa ripoti ya siri ya IAEA

Mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao Vienna amesema, kuhusu kutangazwa katika chombo kimoja cha habari cha Magharibi ripoti ya siri ya hivi karibuni ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, kwamba karibuni hivi Iran italifuatilia kisheria na kwa uzito mkubwa suala hilo.

Kazem Gharib Abadi amesema, ripoti zote za ukaguzi wa shughuli za nyuklia na za makubaliano ya nyuklia JCPOA na vilevile maandikiano yanayofanywa baina ya Iran na IAEA ni masuala ya siri; na akabainisha kuwa, kwa zaidi ya miongo miwili sasa Iran imekuwa ikiulalamikia na kuufuatilia kisheria wakala huo wa kimataifa wa nishati ya atomiki kuhusiana na utunzaji wa taarifa za siri.

Gharib Abadi ameongeza kuwa, uenezaji wa taarifa zozote za siri kabla ya kufuata utaratibu wake wa kisheria ni suala lililo chini ya mamlaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pekee ikiwa ndio mmiliki na yenye kutoa taarifa hizo.

Siku ya Ijumaa, vyombo vya habari vya Magharibi vilitangaza kuwa, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umezitangazia nchi wanachama wa wakala huo kwamba Iran imeamua kufunga idadi kubwa zaidi ya mashinepewa (centrifuges) za kisasa aina ya IR-2m katika kituo chake cha nyuklia cha Natanz.

Muonekano wa mashinepewa katika kituo cha nyuklia cha Natanz

Hii si mara ya kwanza kwa ripoti za siri za IAEA zinazohusiana na shughuli za nyuklia za Iran kuwekwa wazi katika vyombo vya habari.

Habari hiyo imetolewa ndani ya muda mfupi na kuakisiwa sana na vyombo vya habari vya Magharibi, mara baada ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) kupitisha vipengele vikuu vya mpango wa hatua ya kistratejia ya kuondolewa vikwazo.../