Kimya cha jumuiya na mashirika ya kimataifa; mhamasishaji wa ugaidi wa kiserikali
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i65038-kimya_cha_jumuiya_na_mashirika_ya_kimataifa_mhamasishaji_wa_ugaidi_wa_kiserikali
Mauaji ya kigaidi aliyofanyiwa shahid Mohsen Fakhrizadeh, mwanasayansi bingwa wa masuala ya nyuklia na ulinzi ambaye pia alikuwa Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Iran yamelaaniwa na nchi nyingi duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 06, 2020 06:51 UTC
  • Kimya cha jumuiya na mashirika ya kimataifa; mhamasishaji wa ugaidi wa kiserikali

Mauaji ya kigaidi aliyofanyiwa shahid Mohsen Fakhrizadeh, mwanasayansi bingwa wa masuala ya nyuklia na ulinzi ambaye pia alikuwa Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Iran yamelaaniwa na nchi nyingi duniani.

Dk Mohsen Fakhrizadeh aliuawa shahidi jioni ya siku ya Ijumaa ya tarehe 27 Novemba katika shambulio la kigaidi lililotokea kwenye viunga vya Tehran.

Mashirika, jumuiya na taasisi nyingi za kielimu na watu muhimu huru kimataifa wameonesha kusikitishwa na kukasirishwa sana na mauaji hayo ya kikatili. Hata hivyo yale matumaini ya kulaaniwa vikali jinai hiyo na bila kuzungusha maneno bado hayajatimia.

Ali Bagheri Kani, Katibu wa Kamati ya Haki za Binadamu ya Chombo cha Mahakama cha Iran, siku ya Ijumaa aliwatumia barua tofauti Katibu Mku wa Umoja wa Mataifa na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa umoja huo, na huku akigusia jinai ya kuuliwa kigaidi mwanasayansi bingwa wa nyuklia na masuala yaulinzi wa Iran alilalamikia kutochukuliwa hatua za maana na za kivitendo dhidi ya wahalifu wa ugaidi huo. Alisema: Kimya na udhaifu uliooneshwa kuhusu jinai hiyo ni aina fulani ya kuhalalisha vitendo vya kigaidi na kutia nguvu misimamo mikali.

Wanasayansi wa nyuklia wa Iran waliouawa shahidi kigaidi

 

Amezungumzia pia misimamo ya wazi na  mikali inayochukuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati vinapotokea vitendo vya kigaidi katika nchi nyinginezo kama vile vilivyotokea Austria na Ufaransa. Umoja wa Mataifa ulitoa matamko makali na ya wazi kabisa tarehe 3 Novemba 2020 na tarehe 17 Septemba 2020 kuhusu matukio hayo ya Austria na Ufaransa. Baada ya kuwakumbusha hayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa umoja huo; Bw. Ali Bagheri Kani  amewataka viongozi hao rasmi wa ngazi za juu zaidi wa Umoja wa Mataifa wasifanye ubaguzi kuhusu mauaji ya kigaidi aliyofanyiwa mwanasayansi mkubwa wa Iran, shahid Fakhrizadeh.

Ukweli ni kwamba, nchi zinazojilabu kupiga vita ugaidi, zinatumia kisingizio chochote zinachopata, kutoa madai ya uongo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kudai kuwa eti Tehran inaunga mkono vitendo vya kigaidi. Lakini vinavyotokea vitendo vya kigaidi na kuthibitisha ukweli halisi kwamba Iran ni muhanga mkuu wa vitendo vya kigaidi, wakati huo nchi hizo hazisiti hata kidogo kutia ulimi puani na kufuata siasa za nyuso mbili. Kusema kweli, ni sawa kabisa alivyosema Katibu wa Kamati ya Haki za Binadamu ya Chombo cha Mahakama cha Iran kwamba jamii ya kimataifa imekumbwa na changamoto kubwa kuhusu amani na usalama wa kimataifa kutokana na nchi za Magharibi kuingiza siasa, kufanya ubaguzi na kufuata sera za kindumilakuwili mbele ya jinai za kigaidi.

Ali Bagheri Kani

 

Mara chungu nzima maadui wa taifa la Iran wameonesha kuwa, hawasiti hata chembe kufanya jinai yoyote ile dhidi ya taifa hili la Kiislamu. Mifano iko mingi, wa karibuni kabisa mbali na wa shahid Fakhrizadeh, ni wa kuuliwa kigaidi na kidhulma, Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH). Kila mmoja anaujua mchango mkubwa wa shujaa huyo katika vita dhidi ya ugaidi. Mauaji ya kigaidi wamefanyiwa pia wanayansi wengine kadhaa wa nyuklia wa Iran na magaidi wale wale maarufu wanaoendesha ugaidi wa kiserikali nje ya  mipaka ya tawala zao, lakini jamii ya kimataifa haichukui hatua yoyote ya maana kukabiliana na ugaidi huo wa kimataifa. Hili kabla ya jambo lolote linazidi kuonesha jinsi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilivyo muhanga mkubwa wa vitendo vya kigaidi na kwamba madai ya maadui hao hao wanaolifanyia ugaidi wa kila aina taifa hili la Kiislamu, wanaodai kuwa eti Tehran ni muungaji mkono wa vitendo vya kigaidi, ni maneno chapwa yasiyo na mshitiri.

Inasikitisha kuona kuwa taasisi na mashirika ya kimataifa yanafuata siasa za nyuso mbili kuhusu ugaidi kutokana na kudhibitiwa na lobi za Marekani na Uzayuni wa kimataifa. Jambo la chini kabisa linalotarajiwa lifanywe na taasisi hizo ni kulaani kwa maneno makali vitendo vya kigaidi popote vinapotokea na bila ya kufanya ubaguzi wowote. Kushindwa taasisi hizo za kimataifa kutekeleza majukumu yake katika suala hilo bila ya shaka yoyote kunachochea vitendo hivyo na hapana shaka walimwengu wana hamu ya kuyaona mashirika hayo yakijibu dukuduku lao kwa nini yanashindwa kutekeleza majukumu yao ya kupambana na jinai hizo.