Upayukaji wa viongozi wa Saudia dhidi ya Iran, ndoto za kufilisika kisiasa
Viongozi wa Saudi Arabia ambao siku hizi nyoyo zao zimejaa hofu na woga kutokana na mabadiliko ya kisiasa ya eneo hili na matokeo ya kubwagwa Donald Trump huko Marekani, inaonekana wameshindwa kupata njia nyingine ya kujivua na lawama za kuchochea machafuko na ugaidi katika ukanda huu kwa kutumia fedha na fikra zao za ukufurishaji, ghairi ya kupayuka na kutuhumu watu wengine kwa mambo yasiyo na msingi.
Matamshi ya siku ya Jumamosi yaliyotolewa na Faisal bin Farhan Aal Saud, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia alipohojiwa na France Press ni mwangwi wa kufilisika na kuishiwa huko kisiasa. Katika mahojiano hayo na katika hotuba yake ya siku ya Ijumaa mbele ya baraza la "Mazungumzo ya Ukanda wa Mediterenia" waziri huyo wa mambo ya nje wa Saudia alidai ana wasiwasi na mradi wa nyuklia wa Iran. Aidha alijinata kwamba Riyadh ina nafasi ya kipekee katika matukio ya eneo hili na kujipa uthubutu wa kutaka nchi yake na za eneo la Ghuba ya Uajemi zishauriwe kabla ya kufikiwa makubaliano yoyote yale mapya na Iran. Aidha alirudia kutoa madai yasiyo na msingi dhidi ya Tehran na kudai kwamba Riyadh iko tayari kwa ajili ya mazungumzo kuhusu uzalishaji wa silaha za nyuklia na utumiaji wa makombora ya balestiki. Kwa kweli kujiingiza waziri huyo wa mambo ya nje wa Saudia katika masuala hayo yasiyomuhusu ndewe wala sikio, kunaonesha jinsi ndoto na kuishiwa kisiasa kulivyowatawala viongozi wa Saudi Arabia ambao hawajui wajipapatue vipi kutoka kwenye migogoro waliyojitumbukiza wenyewe. Wanaonesha wazi kuwa, silaha wanayoiona bora kwao ni kueneza chuki dhidi ya Iran katika eneo hilo.
Mchezo huo ni sehemu siasa zilizoshindwa za Saudia na haziwezi kuficha mchango haribifu wa Riyadh katika matukio mbalimbali ya muongo mzima uliopita. Siasa za kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine kupitia kuanzisha miungano na kuanzisha vita vya niaba katika nchi za Waislamu kama Iraq na Syria, kuunga mkono magenge ya kigaidi yanayofanya jinai katika kona mbalimbali kiasi kwamba Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia alifikia kutangaza wazi lengo lake la kuchochea machafuko na umwagaji wa damu ndani ya Iran, kuongoza vita angamizi na vya kikatili dhidi ya taifa maskini la Kiislamu na Kiarabu la Yemen, kuingilia na kuzima mapinduzi ya wananchi katika nchi mbalimbali za Kiarabu kama vile Misri na siasa nyingine nyingi haribifu zinazofanywa na viongozi wa Saudia, si mambo ambayo yanaweza kutatuka kwa kubwabwaja na kutuhumu watu wengine kwa mambo yasiyo na mashiko. Upayukaji huo hauwezi kamwe kuwavua na lawama viongozi wa Riyadh katika jinai na vita dhidi ya Yemen, kuunga mkono magenge ya kigaidi kifedha na kifikra, kupigania kwake uhusiano wa kawaida na utawala katili wa Israel na pia kusaliti malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina na Kibla cha Kwanza cha Waislamu.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuna nukta mbili kuu za kuzingatiwa katika upayukaji huo wa viongozi wa Saudi Arabia.
Mosi ni kujaribu kwao kuficha sura halisi ya Saudia ya kuvuruga utulivu na kuzusha machafuko katika eneo hili.
Pili ni kujaribu kwao kuficha shughuli zisizo za kawaida za nyuklia za Saudi Arabia kupitia kutoa madai ya uongo kuhusu mradi wa amani wa nyuklia wa Iran. Olli Heinonen, naibu wa mkuu wa zamani wa wakaguzi wa silaha za nyuklia wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Haward cha nchini Marekani anasema: Saudi Arabia si muwazi katika miradi yake ya nyuklia na sisi hatujaona miradi ya nyuklia iliyo wazi na wadhiha ya Riyadh zaidi ya kutaja tu vinu vya nyuklia ambavyo inaomba ijengewe.
Tajiriba ya huko nyuma imethibitisha kwamba kutoa matamshi ya kuropoka na kuzusha fitna na mizozo hakusaidii chochote katika juhudi za kuleta amani na utulivu. Huenda viongozi wa Saudia wamesahau kwamba Marekani kwa miaka mingi inafanya njama za kuitangaza Iran kuwa ni tishio wakati hiyo hiyo Marekani inaishochea Riyadh kuanzisha vita na migogoro katika eneo hili. Kwa kuzingatia yote hayo tutaona kwamba, viongozi wa Saudia hawako kabisa katika nafasi ya kujifanya wao ni washauri wala kukjipa uthubutu wa kuingilia mambo yasiyowahusu na hawana hadhi ya kupotosha ukweli kuhusu manufaa ya kitaifa na kiulinzi ya Iran wala kuweka masharti yoyote kuhusu hatima ya mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA.