Raisi: Uistikbari wa Marekani unajumuisha Wademocrat na Warepublican
Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema uistikbari na ubeberu wa Marekani unajumuisha vyama vyote viwili vikuu nchini humo vya Democratic na Republican na kuongeza kuwa, ni Iran yenye nguvu tu inayoweza kukabiliana na uistikbari.
Sayyid Ibrahim Raisi Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo Jumapili kwa mnasaba wa kuwadia Siku ya Wanachuo. Akihutubu wakati alipokutana na wawakilishi wa jumuiya za wanachuo mjini Tehran amesema: "Marekani imedhoofika zaidi leo kuliko ilivyokuwa mwaka 1953. Kashfa ya Marekani leo inaonyesha wazi kuwa hakuna chohote kinachoweza kufichwa na kila siku kashfa zaidi zinafichuka."
Aidha Raisi amesema leo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepata nguvu katika eneo zaidi ya wakati wowote mwingine ule na kuongeza kuwa: "Kile ambacho kinaikatisha tamaa Marekani ni Iran ya Kiislamu yenye nguvu."
Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, Shahidi Mohsen Fakhrizadeh, msomi bingwa wa sekta za nyuklia na ulinzi Iran alikuwa nembo ya kusambaratisha vitisho na vikwazo vya adui na kuongeza kuwa, kupinga uistikbari na ubeberu ndiyo siri ya heshima ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Itakumbukwa kuwa miaka 67 iliyopita , yaani Disemba 7 mwaka 1953, wanachuo wa Chuo Kikuu cha Tehran walifanya maandamano ya kupinga kuja nchini Iran Makamu wa Rais wa Marekani wakati huo, Richard Nixon. Askari wa Shah waliua wanachuo watatu katika maandamano hayo. Safari hiyo ilifanywa na Nixon miezi mitatu na nusu baada ya Marekani kufanya mapinduzi ya kijeshi yaliyoipindua serikali ya Dk Mosaddiq. Siku hii imetangazwa kuwa ni Siku ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini Iran kutokana na umuhimu wake mkubwa.