Vifaa vya satalaiti vilitumika katika mauaji ya kigaidi ya Shahidi Fakhrizadeh
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema mauaji ya Mohsen Fakhrizadeh, mwanasayansi bingwa wa Iran yalifanyika kwa kutumia vifaa vya kisasa vya kieletroniki vilivyokuwa vikiongozwa kwa satalaiti. Ameongeza kuwa, Wazayuni wanafahamu vyema kuwa jinai yao hiyo haitabaki bila kujibiwa.
Dk Mohsen Fakhrizadeh, Mkuu wa Shirika la Utafiti na Ubunifu la Wizara ya Ulinzi ya Iran ambaye pia alikuwa msomi bingwa wa nyuklia aliuawa shahidi jioni ya siku ya Ijumaa ya tarehe 27 Novemba katika shambulio la kigaidi lililotokea kwenye viunga vya Tehran.
Akizungumza katika kikao cha kumuenzi Shahidi Fakhrizadeh ambacho kimefanyika Jumapili katika mji wa Bandar Abbas kusini mwa Iran, Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jenerali Ramadhan Sharif ameashiria kujitolea muhanga timu ya walinzi wa Shahidi Fakhrizadeh na kuongeza kuwa: "Wazayuni wanafahamu vyema kuwa kitendo chao hicho hakitabaki bila kujibiwa na hilo limethibitika katika miaka ya hivi karibuni."
Jenerali Ramadhan Shariff amesema baada ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, maslahi ya Marekani na Wazayuni yaliingia hatarini na Wazayuni wamekuwa wakilitazama taifa adhimu la Iran kuwa kizingiti katika jinai na sera zao za kujitanua.
Msemaji wa IRGC amesema Wazayuni maghasibu hawana mizizi ya ustaarabu na kuongeza kuwa utawala bandia wa Israel, katika kipindi cha miaka 70, umewaua wasomi 2700 wa nchi za Kiislamu katika eneo. Amesema utawala wa Kizayuni wa Israel unajifakharisha kwa kufanya mauaji hayo na hata umechapisha majina ya wasomi hao katika vitabu kadhaa.
Jenerali Ramadhan Shariff amesema lengo kuu la Wazayuni ni kuzuia nchi za Kiislamu hasa Iran kufika katika kilele cha sayansi lakini amekumbusha kuwa, kwa baraka ya damu ya mshahidi, Iran ya Kiislamu imeweza kupata mafanikio mengi ya kisayansi.