Zulnouri: Wakala wa IAEA unampatia adui taarifa za Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i65068-zulnouri_wakala_wa_iaea_unampatia_adui_taarifa_za_iran
Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje Katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislam ya Iran (Bunge) amesema kuwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) unampatia adui taarifa za Iran na wala haulindi amana katika marhala mbalimbali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 08, 2020 02:46 UTC
  • Zulnouri: Wakala wa IAEA unampatia adui taarifa za Iran

Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje Katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislam ya Iran (Bunge) amesema kuwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) unampatia adui taarifa za Iran na wala haulindi amana katika marhala mbalimbali.

Mojtaba Zulnouri ameongeza kuwa, baadhi ya wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) ni majasusi wa nchi za Magharibi; ambao huku wakitumika kama wawakilishi wa wakala huo wanayapatia taarifa za siri za Iran mashirika ya kijasusi ya adui. Mojtaba Zulnouri aliyasema hayo jana akijibu kufichuliwa ripoti ya siri ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia kuhusu Iran. 

Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje Katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislam ya Iran ameashiria kupasishwa katika Majlisi hiyo muswada kwa jina la "Strategic Action Plan to Lift Sanctions" na kueleza kuwa, kupasishwa mswada huo utazuia hatua za kijasusi za maadui wa Jamhuri ya Kiislamu. 

Kazem Gharibabadi Balozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu katika taasisi za kimataifa zenye makao yake huko Vienna Austria pia Jumamosi iliyopita aliashiria kutolewa kwenye vyombo vya habari vya Magharibi ripoti ya siri ya hivi karibuni ya IAEA  na kueleza kuwa Iran karibuni hivi itafuatilia kwa jadi kisheria suala hilo. 

Kazem Gharibabadi, Balozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu katika taasisi za kimataifa zenye makao yake huko Vienna Austria

Vyombo vya habari vya Magharibi Ijumaa iliyopita vilitangaza kuwa, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki umezitangazia nchi wanachama wake kwamba, Iran ina mpango wa kufunga sentrifuji zaidi za kisasa aina ya IR-2M katika taasisi yake ya nyuklia ya Natanz. Hii si mara ya kwanza kuvuja katika vyombo vya habari ripoti za siri za wakala wa IAEA kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran. Huko nyuma pia Mikhail Ulyanov Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Taasisi za Kimataifa zenye makao yake mjini Vienna Austria aliwahi kulalamikia kuvuja ripoti za siri za wakala wa IAEA kwenye vyombo mbalimbali vya habari.