Vifo vya Covid-19 vyaendelea kupungua nchini Iran
Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran amesema kuwa, watu wengine zaidi ya elfu 8 wameambukizwa virusi vya corona na wengine 221 wamefariki dunia kwa Covid-19 katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Bi Sima Sadat Lari ameeleza hayo leo wakati akitoa takwimu za karibuni kabisa za maambukizi ya corona hapa nchini na kuongeza kwamba, kwa mujibu wa matokeo ya vipimo rasmi walivyofanyiwa watu katika muda wa masaa 24 yaliyopita wagonjwa wapya 8,201 waliokumbwa na ugonjwa wa COVID-19 wamegunduliwa humu nchini, ambapo 1,286 miongoni mwao wamelazwa hospitalini na waliobakia wamepatiwa huduma za tiba na kurudi nyumbani.
Aidha Dakta Lari amesema kuwa, idadi ya watu waliogunduliwa kupatwa na ugonjwa wa COVID-19 nchini Iran hadi hivi sasa imefikia 1,100,818 na kuongeza kuwa kufuatia wagonjwa 221 kuaga dunia katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, jumla ya watu waliofariki dunia hadi sasa hapa nchini kutokana na ugonjwa huo imefikia 51,949
Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran ameongeza kuwa hadi sasa watu 800,853 wamepona maradhi ya Covid-19 hapa nchini na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, vifo na maambuzi ya corona nchini Iran yameendelea kupungua katika siku za hivi karibuni kufuatia kanuni na sheria kali zinazotekelezwa na serikali ikishirikiana na Kamati ya Taifa ya Kupambana na Covid-19.
Marekani imeendelea kuwa nchi iliyoathiriwa zaidi na corona ambapo karibu watu milioni 16 na nusu wameaambukizwa virusi hivyo huku zaidi ya laki tatu wakiwa wameaga dunia kwa Covid-19 nchini humo.