Mwanga wa matumaini wa hati ya makubaliano ya pande kadhaa ya ‘Chabahar’
Kutumia uwezo wa kieneo ni moja ya mbinu na njia za ushirikiano wa pande kadhaa ambazo zina nafasi muhimu sana katika kupanua ustawi na maendeleo.
Katika fremu hii, kikao cha kwanza cha pamoja cha kundi la nguvukazi la Iran, India na Uzbekistan kimefanyika Jumatatu ya leo tarehe 14 Desemba kwa njia ya mawasiliano ya Intaneti ambapo pande tatu zimejadili namna ya kustafidi na bandari ya kistratejia ya Chabahar.
Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya India kuhusiana na kikao hiki cha pande tatu ilitolewa siku moja baada ya Rais Shavkat Mirziyoyev wa Uzbekistan kufanya mazungumzo kwa njia ya mawasiliano na Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India Ijumaa iliyopita ambapo wawili hao walisisitizia ulazima wa kufanyika kikao hiki cha pande tatu na Iran kuhusiana na Bandari ya Chabahar.
Bandari ya Chabahar daima imekuwa na umuhimu mkubwa katika ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa wa eneo. Kwa upande wa jiopolitiki, Chabahar inahesabiwa kuwa bandari pekee ya bahari nchini Iran ambayo ni nukta muhimu katika Ukanda wa Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman ambayo kimsingi ina nafasi muhimu na ya kistratejia katika korido ya Kaskazini-Kusini.
Umuhimu wa kistratejia wa hati ya makubaliano ya pande tatu ya Chabahar, hivi sasa baada ya kupita miaka minne tangu ilipotiwa saini Juni 2016 umedhihirika zaidi. Hatua ya Uzbekistan ya kuwa tayari kujiunga na hati hiyo ya makubaliano na hamu ya mataifa mengine ya eneo katika uwanja huu ni ishara ya wazi ya kuweko mwanga wa matumaini wa ushirikiano huu.
Gazeti la Hindustan Times limeashiria katika ripoti yake shughuli za India katika Bandari ya Chabahar pamoja na miradi ya uwekezaji ya nchi hiyo katika bandari hii ya Iran na kuandika: Kutokana na umuhimu wa Bandari ya Chabahar katika kusafirisha bidhaa kuelekea Afghanistan, Marekani imelazimika kutoijumuisha bandari hii muhimu katika orodha ya vikwazo vyake.
Ukweli wa mambo ni kuwa, kutegemeana na kuweko mahitaji ya pande mbili, ni nukta ambayo inaleta udharura wa kupanua na kustawisha bandari hii muhimu na kuvifanya vikwazo kutokuwa na maana.
Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India alisoma beti za mashairi ya malenga mashuhuri wa Iran Hafez Shirazi katika hafla ya utilianaji saini hati ya makubaliano ya pande tatu na kusema bayana kwamba: Zama za kutengana na nyusiku za kufarakana zimefikia kikomo na urafiki wetu utaendelea daima.
Aidha Waziri Mkuu huyo wa India alisema wazi kwamba: Mkataba wa kuanzisha korido ya pande tatu ya Chabahar unaweza kubadilisha njia na mustakabali wa eneo hili na wakati huo huo kuweka misingi ya njia mpya katika eneo, kama ambavyo korido hii inaweza kuondoa vizingiti vya harakati ya kiuchumi katika eneo lote.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatambua kuwa, usalama, uthabiti na ustawi wa kiuchumi wa mataifa ya eneo na majirani ni usalama na ustawi wake. Ni kutokana na ukweli huo, ndio maana Iran imetangaza utayari wake wa kutumia suhula na uwezo wake ikiwa kama moja ya vituo muhimu vyenye utajiri wa nishati na njia kuu za mawasiliano ya eneo kwa minajili ya kusukuma mbele gurudumu la uchumi wa pamoja kama vile kusaidia kusafirisha nishati na kuruhusu upitishwaji wa bidhaa za mataifa mengine katika ardhi yake kuelekea mataifa mengine.
Katika harakati hii nzuri, kunufaika na uwezo wa Bandari ya Chabahar kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha korido ya Kaskazini-Kusini ni fursa ambayo inaweza kuzingatiwa na kutumiwa kwa ajili ya kufikia malengo yaliyoainishwa na mataifa husika.