Iran yaitaka Marekani iondoe askari wake vamizi nchini Syria
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema vikosi vamizi vya nchi ajinabi vikiweko vya Marekani vinapaswa kuondoka nchini Syria mara moja.
Majid Takht-Ravanchi alisema hayo jana Jumatano katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliojadili matukio ya Asia Magharibi ukiwemo mgogoro wa kibinadamu na kisiasa wa Syria na kusisitiza kuwa, vikosi hivyo vamizi vipo nchini Syria kinyume cha sheria, na vinapaswa kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Kadhalika ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuiunga mkono na kuisaidia serikali ya Damascus katika kupambana na magaidi na wavamizi.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran amesisitiza kuwa, Tehran imejitolea kwa dhati kuhakikisha kuwa mgogoro wa Syria unapatiwa ufumbuzi kwa njia za kisiasa na kidiplomasia.
Makundi ya kigaidi yenye mfungamano na Marekani na Uturuki yamepiga kambi kinyume cha sheria katika maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki ya Syria, ambapo mbali na kupora maliasili ya mafuta ya nchi hiyo yanachukua hatua pia dhidi ya wakazi na vikosi vya jeshi la Syria katika maeneo hayo.
Serikali ya Damascus imesisitiza mara kadhaa kwamba magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani na vikosi vyenye mfungamano nayo yanapaswa yaondoke katika maeneo hayo.