Hakuna mazungumzo mapya yatakayofanyika kuhusu JCPOA
Mapatano ya nyuklia ya JCPOA ni mapatano ya kimataifa yaliyofikiwa na pande kadhaa mbazo zinatakiwa kuyatekeleza kivitendo na kwa hivyo mapendekezo ya upande mmoja ya kutaka mazungumzo mapya yafanyike katika uwanja huo ni jambo lisilowezekana.
Kazem Gharib Abadi, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Taasisi za Kimataifa zenye Makao yao mjini Vienna Austria alisema Alkhamisi kwamba tathmini yoyote ya jinsi ya kutekelezwa mapatano hayo bila shaka iko nje ya mamlaka ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA na suala hilo linapaswa kuepukwa.
Gharib Abadi ameendelea kusema: IAEA ilitekeleza jukumu lake wakati wa kufanyika mazungumzo ya JCPOA. Ahadi na majukumu ya kila mwanachama pamoja na IAEA yamebainishwa wazi na kwa umakini mkubwa, jambo ambalo limeafikiwa na wote na hivyo kila upande unafahamu vizuri majukumu unayopaswa kuyatekeleza katika mapatano hayo.
Gharib Abadi ameyasema hayo kufuatia matamshi yaliyotolewa karibuni na Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA mbele ya shirika la habari la Reuters, aliyedai kwamba kuhuishwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA katika kipindi cha uongozi wa Joe Biden nchini Marekani kunahitajia mapatano mapya yatakayoainisha ni jinsi gani uwajibikaji wa Iran unapaswa kurejeshwa katika hali ya kabla ya kupunguza majukumu yake.
Hata hivyo Gharib Abadi aliandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter siku ya Ijumaa kuwa alikutana baadaye na Grossi ambaye alisisitiza kwamba mazungumzo yake na Reuters hayakuwa na maana ya ulazima wa kufanyika mazungumzo mapya na kwamba mahojiano yake kuhusu suala hilo yako wazi kabisa kwa kuwa yalihusiana tu na majukumu ya IAEA.
Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Taasisi za Kimataifa zilizo na Makao yao mjini Vienna Austria amesema kwamba katika mahojiano yake na Reutrs, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA alisema protokali na makubaliano maalumu yanapaswa kuwepo ili pande zote zirejee katika hali ya kabla ya Iran kupunguza uwajibikaji wake, na sio udharura wa kufanyika mazungumzo mapya ya JCPOA.
Jambo linalosahaulika na wengi ni kwamba, Iran ililazimika kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano ya JCPOA kutokana na sababu za kisheria na kimantiki.
Sayyid Jalal Sadatiyan, mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema kuhusu suala hilo kwamba: Ni Ulaya na Marekani ndizo zimeyateka nyara mapatano ya JCPOA na kutoyatekeleza kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu na vilevile kutokana na mabavu yazo; na sio Iran ambayo kwa mujibu wa ripoti chungu nzima za IAEA imetekeleza vizuri majukumu yake.
Mwaka mmoja baada ya kujitoa Marekani katika mapatano ya JCPOA, Baraza Kuu la la Usalama wa Taifa la Iran lilichukua uamuzi wa kusimamisha hatua kwa hatua uwajibikaji wa kujitolea wa Iran katika mapatano ya JCPOA na kwa mujibu wa vipengee vya 26 na 36 vya mapatano hayo. Pamoja na hayo Iran inasisitiza kwamba iko tayri kurejea katika hali ya zamani ya uwajibikaji wake iwapo tu itaondolewa vikwazo na pande nyingine nazo ziwajibishwe kutekeleza majukumu yao katika mapatano hayo.
Kuna malengo mawili makuu yanayofuatiliwa na wachochezi dhidi ya Iran kupitia vyombo vya habari. La kwanza ni kujaribu kuonyesha kwamba IAEA haipewi ushirikiano wa kutosha katika kusimamia miradi ya nyuklia ya Iran, jambo linalokwenfa kinyume kabisa na ukweli wa mambo.
Lengo la pili ni kutumiwa IAEA kutoa mashinikizo dhidi ya Iran ili isalimu amri na kukubali matakwa mapya ya nchi za Magharibi, na hilo ni jambo linalofuatiliwa kwa karibu sana na Marekani na nchi za Ulaya. Tusisahau kwamba baada ya kujitoa katika mapatano ya JCPOA na kuanza kutekeleza siasa za 'mahsinikizo ya juu kabisa', Trump aliahidi kuwa angeilazimisha Iran iketi kwenye meza ya mazungumzo ili kufikia kile alichokitaja kuwa 'mapatano bora', ndoto ambayo ameshindwa kuifikia hata katika siku za mwisho mwisho za utawala wake.
Mbali na uchochezi wa Reuters na upotoshaji wa mahojiano ya Grossi dhidi ya Iran, ni wazi kuwa hakuna mazungumzo mapya yatakayofanyika kuhusu mapatano ya JCPOA na iwapo yatahuishwa hakutakuwepo pia na haja ya kuandikwa protokali au hati mpya ya kuainisha nafasi ya IAEA katika mapatano hayo.