IRGC: Israel itapata jibu kwa jinai zake dhidi ya taifa la Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i66916-irgc_israel_itapata_jibu_kwa_jinai_zake_dhidi_ya_taifa_la_iran
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amesema hakuna chembe ya shaka kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel utapokea jibu kali la Iran kutokana na jinai zake dhidi ya taifa hili, yakiwemo mauaji ya wanasayansi na wasomi wa Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 16, 2021 04:32 UTC
  • IRGC: Israel itapata jibu kwa jinai zake dhidi ya taifa la Iran

Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amesema hakuna chembe ya shaka kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel utapokea jibu kali la Iran kutokana na jinai zake dhidi ya taifa hili, yakiwemo mauaji ya wanasayansi na wasomi wa Iran.

Brigedia Jenerali Ramezan Sharif amesema maadui wanatumia vyombo vya habari katika vita vya kisaikolojia dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu na Mfumo wa Kiislamu unaotawala hapa nchini kwa lengo la kutaka kuvuruga akili na imani ya taifa hili.

Ameeleza bayana kuwa: Utawala bandia na wa Kizayuni bila shaka utapokea jibu kwa vitendo vyake ghalati dhidi ya taifa la Iran. 

Brigedia Jenerali Sharif amekumbusha namna maadui walivyojaribu kupalilia kasumba katika fikra za vijana wa Iran huko nyuma bila mafanikio na kueleza kuwa: Walitaka kuwarubuni vijana kwamba Shah na washauri wake wa Kimarekani wanaipeleka nchi katika ustaarabu mkubwa, lakini Mapinduzi ya Kiislamu yalifelisha njama hizo.

Askari wa SEPAH ya Iran

Amebainisha kuwa, ni wazi kuwa mafanikio ya Iran hayapingiki wala kukataliwa hata na maadui, na kwamba upinzani na uhasama wao mkubwa dhidi ya Mfumo wa Kiislamu ni dhihirisho la nguvu na uwezo mkubwa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, matukio ya hivi karibuni yanaonesha namna Wamagharibi wanavyoporomoka, na kufeli Marekani kueneza ubeberu wake duniani.