Khatibzadeh: Saudia imeliteka nyara Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i68060-khatibzadeh_saudia_imeliteka_nyara_baraza_la_ushirikiano_la_ghuba_ya_uajemi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran usiku wa kuamkia leo amejibu taarifa ya mwisho ya kikao cha hivi karibuni cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na kusema kuwa utawala wa kiimla wa Saudi Arabia umeliteka nyara baraza hilo na unachochea chuki na machafuko katika eneo hili kupitia kutwisha kwake misimamo yake isiyokubalika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 19, 2021 04:35 UTC
  • Khatibzadeh: Saudia imeliteka nyara Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran usiku wa kuamkia leo amejibu taarifa ya mwisho ya kikao cha hivi karibuni cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na kusema kuwa utawala wa kiimla wa Saudi Arabia umeliteka nyara baraza hilo na unachochea chuki na machafuko katika eneo hili kupitia kutwisha kwake misimamo yake isiyokubalika.

Shirika la habari la Tasnim limemnukuu Saeid Khatibzadeh akijibu taarifa ya mwisho ya kikao cha 147 cha mawaziri wa mambo ya nje wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na kusema kuwa, taarifa ya mwisho ya kikao hicho kama ilivyokuwa kwa taarifa za vikao vya huko nyuma, imefumbia macho matukio na mabadiliko yanayotokea duniani na imendelea kufanya ukaidi chini ya mashinikizo ya kisiasa ya utawala wa kiimla wa Saudia.

Amesema, siasa za kueneza chuki dhidi ya Iran zitaendelea kushindwa na amehoji kwa kusema, hivi kuendelea kuwa wakaidi na kushikilia siasa hizo ghalati kwa makumi ya miaka, bado hakujaliamsha baraza hilo na kulifanya likae na kujiuliza je, siasa hizo zimeleta utulivu na amani katika eneo hili?

 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aidha amejibu upayukaji wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na kusema kuwa, kitendo cha baraza hilo kujiingiza katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA ya baina ya Iran na kundi la 5+1 na hatua yake ya kuingiza ndani ya mapatano hayo, masuala yasiyohusika kabisa, ni kichekesho kikubwa.

Amesisitiza kwa kusema: Kama ilivyosemwa mara chungu nzima, mapatano ya JCPOA ni makubaliano ya pande mbili baina ya Iran na wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani, hayalihusu pande nyingine. Ni mazungumzo ambayo yamefanyika na kufikiwa mapatano na kuanza kutekelezwa, hivyo njama za utawala wa kiimla wa Saudi Arabia za kujaribu kujipenyeza kwenye mapatano hayo yasiyouhusu ni kichekesho kinachozidi kuwaonesha walimwengu jinsi watawala wa nchi hiyo walivyozama kwenye ndoto isiyoaguka.