May 12, 2016 15:37 UTC
  • Mashindano ya Qur'ani Tukufu yaanza rasmi Tehran

Baada ya Dk Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) kufungua duru ya 33 ya mashindano ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu jana Jumatano, mashindano hayo yameanza rasmi leo.

Mashindano hayo yameanza kwa kuchuanishwa washindanaji wa kuhifadhi Qur'ani nzima na qiraa na uhakiki wa Qur'ani.

Shirika la habari la IQNA limeripoti kuwa, mashindano ya qiraa na kuhifadhi Qur'ani nzima yamefanyika katika kumbi za hoteli walizofikia washindanaji hao mbele ya majaji wa kimataifa ikiwa ni hatua ya mchujo wa kuchagua watu wa kuingia kwenye ukumbi mkuu wa mashindano.

Itakumbukwa kuwa nchi 75 zina wawakilishi wao katika mashindano hayo. Hayo yamesemwa na Sheikh Ali Mohammadi Mwakilishi wa Faqihi Mtawala na Mkuu wa Taasisi ya Wakfu ya Iran ambaye ameongeza kwamba, kutakuwa na washiriki 130 kutoka nchi 75 katika mashindano hayo.

Amesema kwa mara ya kwanza mashindano hayo yanafanyika katika Ukumbi Mkubwa wa Swala wa Imam Khomeini MA hapa jijini Tehran, ili kuwezesha idadi kubwa ya watu kujumuika katika mashindano hayo.

Sheikh Ali Mohammadi ameongeza kuwa, mashindano ya mwaka huu yatakuwa na washiriki kutoka mabara ya Afrika, Asia, Ulaya, Marekani na Pasifiki.

Mashindano hayo ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yanatarajiwa kumalizika siku ya Jumanne ya mwezi kumi Shaaban, sawa na tarehe 17 mwezi huu wa Mei.

Tags