Iran: Mazungumzo mazuri yanawezekana iwapo Wamagharibi wataonyesha nia njema
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema kufikia mapatano mazuri ni jambo linalowezekana katika mazungumzo yanayonedelea Vienna kuhusu kuondolewa Iran vikwazo lakini akasisitiza kuwa, hilo litawezekana iwapo upande wa Magharibi utaonyesha nia njema.
Akizungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa India, Subrahmanyam Jaishankar Jumaosi, Abdollahian amesema mazungumzo hayo yako katika mkondo sahihi. Aidha amesema Iran ina azma inayotakikana ya kufikia mapatano mazuri.
Mazungumzo kati ya wawakilishi wa Iran na wa kundi la 4+1 linaloundwa na Russia, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuhusu kuiondolea Iran vikwazo yangali yanaendelea huku vikao mbalimbali nyeti na muhimu kuhusu masuala tofauti vikifanyika mtawalia na kwa wakati mmoja.
Ali Bagheri Kani mkuu wa timu ya mazungumzo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Vienna Alkhamisi iliyopita alikuwa na mazungumzo na Enrique Mora Naibu Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya na ambaye pia ni mratibu wa mazungumzo hayo ya Vienna na kama ambavyo alionana pia na Mjumbe wa nchi tatu za UIaya yaani Ufaransa, Uingereza na Ujerumani. Bagheri Kani amesema katika tathmini yake ya karibuni kuhusu mwenendo wa mazungumzo ya Vienna kwamba: mazungumzo yanayoendelea Vienna kuhusu suala la kuiondolea vikwazo Iran ni chanya na yanasonga mbele.
Duru ya nane ya mazungumzo ya Vienna, ambayo ajenda yake kuu ni kuondolewa vikwazo vya kidhalimu na visivyo vya kisheria ilivyowekewa Iran, ilianza mwishoni mwa mwaka uliomalizika.
Marekani ambayo ilijiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mnamo Mei mwaka 2018 iliiwekea Iran vikwazo haramu kufuatia uamuzi wake huo na kusababisha mkwamo kwenye utekelezaji wa mapatano hayo, inashiriki mazungumzo ya Vienna nchini Austria kwa njia isiyo ya moja kwa moja.