Kiongozi Muadhamu: Wairani wamegeuza kuuawa shahidi Jenerali Soleimani kuwa ni fursa
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei amesema maadui walidhani kuuawa shahidi kamanda shujaa katika vita dhidi ya ugaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimaini kungekuwa tishio kwa Iran lakini watu wa Iran wamegeuza tukio hilo kuwa fursa kutokana na imani yao ya kidini.
Kiongozi Muadhamu ameyasema hayo katika hotuba aliyotoa leo kwa mnasaba wa mwamko wa wananchi wa Januari 9, 1978 katika mji mtakatifu wa Qum dhidi ya utawala wa zamani wa Shah Pahlavi ambao ulikuwa unapata himaya ya Marekani.
Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa: "Mahesabu mabovu ya Marekani yangali yanaendelea na mfano wa hilo ni kuuawa shahidi Shahidi Soleimani."
"Walidhani kwa kumuondoa shahidi huyu harakati adhimu ya taifa la Iran ingezimwa lakini tuliona harakati kubwa iliyojiri wakati wa maadhimisho ya mwaka wa pili wa kuuawa kwake shahidi."
Amesema nyuma ya mwamko huo wa wananchi ni mkono wa Mwenyezi Mungu.
Aidha amesema mfumo ambao maadui wanatumia kufanya mahesabu yao umevurugika na hawawezi kuwa na tathmini sahihi kuhusu Jamhuri ya Kiislamu na hivyo wataendelea kufeli mara kwa mara.
Ayatullah Khamenei ameendelea kusema kuwa uhasama wa kina wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatokana na itikadi za kidini.
Taarifa zaidi kuhusu hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu itakujieni katika matangazo yetu yajayo.